Siri nzito ya walemavu wanavyoteseka Dar.
INASIKITISHA na kuleta huzuni ndani ya moyo wako pale unapojikuta
unawapoteza wazazi wako wote huku ukikosa msaada kutoka kwa ndugu wa
karibu na kuamua kujiunga na kundi la ombaomba barabarani.
Baadhi ya watu wanao kuwa wakiomba msaada hasa wale walemavu wa viungo
mbalimbali wa mwili wamekuwa wakileta huzuni kwa wapiti njia kutokana na
ulemamavu wao ambao ni mipango ya Mungu.
Sote ni mashahidi kuwa baadhi ya walemavu wa mikono, miguu, vipofu na
viungo vingine wakiomba msaada kwa madereva, watembea kwa miguu na
kwenye ofisi za Serikali na binafsi na maeneno mengine.
Lakini wapo wengine ambao hawana tatizo lolote lakini wameamua kuingia
katika kundi hilo jambo ambalo limekuwa likizua maswali ya kwamba
kwanini wasijishughulishe na biashara ndogondogo.
MTANZANIA Jumatatu ilifanya mahojiano na mlemavu mmoja wa miguu yote
ambaye amekuwa akitembea mithili ya mnyama mwenye miguu minne wakati
akiomba msaada katika kituo cha daladala Ubungo.
Mlemavu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Yusuph Said (24) mzaliwa wa
Kijiji cha Mikese mkoani Morogoro anaeleza maisha anayoishi eneo la
Manzese Darajani jijini Dar es Salaam ambayo ni hatari kwa usalama wa
uhai wake.
Said ambaye alisoma Shule ya Msingi Kitega na baadaye kujiunga na
Sekondari ya Mikese zote za mkoani Morogoro anaeleza kwamba alikimbiwa
na ndugu zake baada ya wazazi wake wote kufariki 2000 kutokana na
maradhi mbalimbali.
Akizungumza kwa huzuni ya kuwapoteza wazazi wake ambao walikuwa wanamlea
kulingana na hali yake ya ulemavu alijikuta akikosa mtu wa kukaa naye
kitendo kilichomfanya kukimbilia kwa shangazi yake Muhombola Salum.
Said anasema alikimbilia kwa shangazi yake baada ya ndugu zake wa
kuzaliwa tumbo moja kumkimbia na kuanzisha maisha yao maeneo mengina
huku shughuli zao kubwa ni kuchoma mkaa porini.
Anasema maisha kwa shangazi yake yalizidi kuwa magumu kutokana na
kutokuwa na uwezo kwani uhakika wa kula kila siku haukuwapo ambapo
alishindwa kuvumilia njaa na kukimbilia Dar es Salaam baada ya kupata
taarifa kuwa walemavu wanapata msaada barabarani kwa kuombaomba.
Hakika, ukimtazama Said hali yake ni vigumu kuvumilia kumsikiliza au
kumwangalia kwani mwili wake unaonekana kutooga siku nyingi, nguo chafu,
shuka analojifunika chafu ana anatembea nalo muda wote kwa kuhofia
kumwibia.
Pia inadhihirisha kabisa ameanza kuathirika kisaikolojia kutokana na
mazingira anayoishi na inathihirisha wazi ameanza kutumia dawa za
kulevya.
Said ambaye alikataa kuweka wazi vitendo wanavyofanyiwa walemavu
wanaoishi eneo la Manzese Dar es Salaam nyakati za usiku kwa kuhofia
maisha yakwe, anasema anatamani kurudi nyumbani lakini anashindwa wapi
atafikia.
“Pale Manzese kuna masela wengi sana, wanatufanyia mambo mengi lakini
siwezi kuyataja hapa naogopa na ndio maana sisi walemavu tumejitenga
na banda letu.
“Hii ni shuka ninayojifunika natembea nayo muda wote kwa ukiachaa
unaibiwa, kuoga kwangu au kufua nguo hizi mara nyingi ninasubiri mvua
inaponyesha.
“Mimi nilikuwa nalelewa na wazazi wangu bila kutekeseka na walikuwa
wameninunulia baiskeli lakini walipofariki iliharibika na hakuna
aliyenitengenezea lakini nashukuru hadi leo naishi kwa msaada wa watu.
“Ukiamua kuwahoji wapiga watu tunaolala nje watakueleza mambo mengi
sana, kuna vituko tunafanyiwa sio kwmaba tunapenda ni kwa sababu huna
jinsi,”anasema kwa masikitiko.
Said anasema kwamba kutokana na kukaa kituoni tena juani kwa kuomba pesa
abiria, madereva na makondakta amekuwa akiugua kila siku lakini baada
ya kupata kiasi hutenga kwa kula chakula na kununua dawa la kutuliza
maumivu.
Anasema kwamba anahofia kwenda hospitali kutibiwa kwa kile alichodai
hatapewa fursa ya kupata matibabu kwa sababu ya pesa na hali yake
ilivyo.
Anasema kwa siku inaweza kupata Sh 5,000 lakini kutokana na mazingira
anayoishi hazitoshi na kuongeza kwmaba pengine hunyang’anywa na masela
nyakati za usiku.
Anaeleza kwamba mbali ya kunyang’anywa fedha pia kupokonywa simu jambo
ambalo linamfanya kutonunua simu, nguo au kutunza fedha za ziada.
Anasema kutokana na hali hiyo hulazimika kuchimba shimo na kufukia
baadhi ya fedha zake anazopata kutoka kwa watu wanaoguswa na hali yake.
Said aliwataja baadhi ya ndugu wa kuzaliwa ni pamoja na Oluka, Salum,
Hiari, Shukuru na Hamis ambao wapo porini wakiendesha shughuli zao za
kukata miti na kuchoma mkaa mkoani Morogoro.
Pamoja na mambo ya Said lakini ombi lake kubw ani kuiomba Serikali
kumsaidia baiskeli ya kutembelea au kumpeleka katika kituo chochote za
kulelea watu wasio na uwezo.
Said anasema mbali ya kumpeleka kituoni, anaomba msaada wa fedha ili
kuanzisha biashara ndogo ambazo anaweza kusifanya kwa kutumia mikono
ambayo haina ulemavu wowote.
Ni dhahiri kwamba Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto inapaswa kutambua
matatizo yanayowapata watu wanaojihusisha na ombaomba barabarani.
Inagawa ni vigumu Serikali kuwachukua watu wote walio mitaani na
kuwatunza lakini kuja haja ya kuchukulia uzito kwa watu wenye ulemavu
hata kwa kuwapeleka katika vituo vya kulelea watu wasio na uwezo.
Si kwamba walemavu wote wanapenda kukaa kwenye vituo hivyo la hasha,
bali wengine wanataka kupata msaada wa fedha ili kuanzisha biashara
ambayo wanaweza kuifanya kulingana na mazingira yao.
Pia Serikali inapaswa kuweka wazi juu ya huduma kwa walemavu katika
hospitali za umma ili waweze kupata huduma bure kwa sababu ya hali zao
ambazo haziwawezeshi kupata kipato cha kujikimu, hii itasaidia pale
wanapougua walemavu waweze kupata matibabu kwa sababu wana haki sawa.
Walemavu wanapoachwa bila kupewa huduma ni moja ya sehemu ya kuwafanyia
ukatili. Sote tunafahamu ukatili ni vitendo vya makusudi vinavyofanywa
na mtu au kikundi dhidi ya mtu, watu wengine ambavyo huwa na madhara ya
kimwili, kiakili na jisaikolojia.
Dhana hii haimanishi kuuawa kwa binadamu pekee bali ukatili unaweza
kujitokeza katika sura tofauti na maneno mbalimbali kama ukatili wa
nyumbani, kiuchumi, kimila na desturi katika makabila, mahusiano ya
kimapenzi, usafirishaji haramu wa binadamu, vitisho na matumizi ya
kutumia nguvu.
Hivyo watu walio barabarani wakiomba msaada wa kusaidia wapo katika
kundi la ukatili wa kiuchumi ndio uliowafanya kuingia barabarani
kujipatia riziki zao.
Kwa mujibu wa Said amesema kwamba nyakati za usiku hufanyiwa vitendo
vya ajabu ambavyo hakuta kuvieleza wazi, lakini kwa akili ya kawaida
inadhihirisha kundi hilo linateseka sana .
Ukatili unaweza kutoka katika kundi lolote ndani ya juamii ikiwa ni kwa
mwanamke, mwanaume, mvulana, msichana au mototo.
Ili kutambua madhara ya ukatili wa kijinsia kwa walengwa hao ni muhimu
kufanya linalowezekana kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kuanzia
ngazi ya familia hadi taifa kuona kila binadamu ana haki katika hali
yoyote ile.
Ingawa mateso wanayopata walemavu barabarani jamii imekuwa
ikiyachukulia pengine ni uamuzi wa mtu kupenda kuingia katika kundi hilo
lakini sivyo ilivyo bali inalazimu kutokana na hali halisi ya maisha.
Umefika wakati sasa wizara, idara, taassi na kampuni binafsi kuona kundi
la walemavu ni moja ya watu wanaopaswa kusaidiwa katika kila hali kwa
sababu hayo ni mapenzi ya Mungu.
Pia vitendo vya baadhi ya familia kuwatelekeza watoto wanaozaliwa kwa
ulemavu au kupata ulemavu wakiwa watu wakubwa ni jambo la kikatili , ni
vema mlemavu akadhaminiwa kama ilivyo kwa wengine.
Maoni 0769 688 300
No comments:
Post a Comment