IMEGUNDULIKA kuwapo na mtandao hatari nchini unaohusisha Hazina na
Halmashauri mbalimbali kuchota mamilioni ya fedha huku wakiziandikia
kutumika katika miradi ya maendeleo.
Mtandao huo ambao umeelezwa kuwahusu viongozi ngazi ya juu wa Hazina na
Halmashauri umekuwa ukiongeza fedha za ziada kati ya Sh. Milioni 500
hadi 600 kwenye fedha halali za miradi ya maendeleo zilizoidhinishwa
kisheria na Bunge.
Tayari mtandao huo umedaiwa kufanikiwa kuidhinisha mamilioni ya fedha
katika Halmashauri tatu ambazo ni Mbarali, Korogwe Mjini na Mvomero.
Hayo yalielezwa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), Rajab Mohamed Mbarouk
alipokuwa akifanya majumuisho ya vikao vya kamati yake.
Mbarouk alisema kumeibika mtandao hatari wa kujichotea fedha za Serikali
kwa kusingizia zinakwenda Halmashauri lakini zinapofikishwa huko
zinawarudia wenyewe.
“Hii nchi sio masikini na hakuna sababu ya kusikia eti miradi imekwama
kwa sababu ya fedha kukosa, katika vikao vyetu tumebaini kwamba Hazina
na Halmashauri nchini zinashirikiana kula fedha za Serikali.
“Mfano halisi ni huu Halmshauri ya Mbarali katika mahesabu yamahitaji
yao yote walitakiwa kupewa Sh. milioni 70 lakini Hazina walipeleka Sh.
milioni 700.
“Fedha hizo zinapofikishwa kule zinaidhinishwa kupokelewa Sh. milioni 70
zilizokuwa zikihitajika zile zilioongezwa zinazrudi mikononi mwa
mtandao huo ambao ni katika Hazina na Halmashauri.
“Halmashauri ya Mbarali imekuwa imekuwa ikipata hati chafu mpaka leo
ninavyoongea hapa katika kuboroga kwenye mahesabu yao ya fedha
wanazopokea na jinsi wanavyozitumia.
“Kama unataka kuona mtandao huo umeota mizizi mikubwa, tumebaini
utakaswaji wa fedha umefanyika Halmashauri ya Korogwe Mjini Sh.milioni
500 huku mahitaji yao yakiwa chini ya Sh. milioni 100.
“Hivyo hivyo utakaswaji huo umefanyika Halmshauri ya Mvomero kwa
kupelekea Sh. milioni 500 ambapo mahitaji yao hayakuwa yanafikia kiasi
hicho, kama wana kamati tumechukizwa na utoroshwaji wa fedha hizo na
tutalifikisha bungeni kwa hatua zaidi.
“Cha ajabu unakuta viongozi wanaohusika katika Halmashauri hizo
wanapofanya utakaswaji huo wanawahi kuhama, mfano halisi ni aliyekuwa
Mhasibu wa Halmshauri ya Mvomero,Nassoro Mkwanda ambaye hivi sasa yupo
Halmshauri ya Kiteto kwa cheo hicho hicho,”alisema.
Mbarouk alisema kama mtandao huo hautadhibitiwa haraka taifa litaendelea
kufilisika na maendeleo ndani ya jamii yakikwama ambapo athari yake ni
uchumi kushikiliwa na wachache huku kundi kubwa ni masikini.
Mkurugenzi Kiteto amwaga machozi
Awali ya yote, Kamati ya LAAC ilikutana na viongozi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Kiteto kupitia mahesabu yao ambapo ilikubaini ubadhirifu
mkubwa wa fedha kitendo kilimfanya Mkurugenzi halmashauri hiyo, Jane
Mutagurwa kulia ndani ya kikao.
Kugundulika kwa ubadhiri katika Halmshauri hiyo kulimfanya Mwenyekiti wa
LAAC, Mbarouk kuagiza polisi kufika hapo ili kuwaweka chini ya ulinzi
baada ya kikao kumalizika.
Kamati ilibaini Halmashauri ya Kiteto imepoteza Sh. milioni 500 ambazo
ambazo ni mapato ya kodi za mazao kutoka kwa vyama vya ushirika.
Ilibainika fedha hizo zilichukuliwa na wakala wa ukusanyaji wa ushuru
huo kwa idhini ya Halmashauri hilo kwa mkataba wao lakini wakotomea bila
kuzikabidhi.
Katika mahojiano kati ya wabunge wa kamati ya LAAC na viongozi wa
Halmashauri hiyo ilibainika kuwa kuna magari mawili ya Serikali yenye
usajili wa STK hayajulikani yalipo na anayeyamiliki licha ya kuonekana
kwenye vitabu vyao ni mali zao.
Pia ilibainika kuwa Sh. milioni 179 zimeanzwa kulipwa kwa watumishi
wanaoidai Halmashauri hiyo lakini hawajulikani kwa majina wala idara
zao.
Vile vile imegundulika kwamba Halmashauri hiyo imekutumia Sh.milioni 34
zilizotokana na mauzo ya mahindi ya msaada wa njaa iliyoikumba Wilaya ya
Kiteto na hazijawahi kurudishwa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Ubadhirifu mwingine uliopatikana katika Halmashauri hiyo ni ujenzi wa
jiko la kisasa lililogharimu Sh. milioni 25 lakini limeshindwa kutumika
na badala wameligeuza kuwa nyumba ya mwalimu huku taarifa zao zikieleza
vitu vyote vimekwekwa kumbe ni uongo.
Hata hivyo ilibainika mamilioni ya fedha yanayotengwa na Serikali
kwemnda miradi mbalimbali ya maendeleo vijijini na mfuko wa kuwawezesha
wanawake na vijana hayawafikii ipasavyo.
Ilibainika miradi mingi ya ujenzi wa shule za msingi na Sekondari
ikiwani ya Kiperesi ikishindwa kukamilika huku fedha zilizotengwa zikiwa
zimetolewa kitendo ambacho kiliwafanywa wajumbe wa LAAC kupendekeza
kuvunjwa kwa Halmshauri hiyo.
Wakati Mkurugenzi, Mutagurwa alipotakiwa kutoa majibu ubadhiri huo
alipatwa na wasiwasi na kigugumizi kueleza wazi na kuanza kulia.
Viongozi wengine waliokuwa wamsaidia kujibu hoja ni Ofisa Mipango wa
Halmashauri hiyo,Rabson Magesa, Mwenyekiti wa Halshauri ya Wilaya ya
Kiteto, Mainge Lemalali na viongozi wengine ambao ilionekana kumsukimia
mkurugenzi wao.
Kutokana na kutokuwapo na majibu sahihi, Mbarouk alimua kuwatoa nje
viongozi wengine ispokuwa Mkurugenzi ili kuhoji peke yake ambapo
ilibainika kwamba viongozi waliomzunguka wanamhujumu huku jamii ya
wamasai wakimdharau ni jinsia yake ya kike.
Mbarouk aliamua kusiktisha mpango wa kumweka chini ya ulinzi wa polisi
baada ya kuelezwa hivyo na kuamua kuunda kamati ndogo ya kuchunguza
ubadhirifu na hali halisi ilivyo Kiteto.
Pia alipewa muda wa kuhajikisha fedha pamoja na gari mbili zinapatikana
kabla ya Disemba 31, mwaka huu ingawa aliomba kuongezewa muda hadi Juni
2014 kitendo kilichopingwa vikali.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment