Thursday 20 February 2014

MTOTO AVUNJWA MGUU KISA ANAKOJOA KITANDANI



Ukatili  huu utaisha lini Kanda ya Ziwa?
*Mtoto avunjwa mguu kisa anakojoa ovyo

Na Benjamin Masese, Mwanza
ILE kauli ya kwamba ‘Uchungu wa mwana aujuaye mzazi’ inakosa uhalisia wake kutokana na  vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kutokea maeneo mbalimbali ya nchi.
Sote tunafahamu watoto ambao ni tegemeo la  taifa la kesho wamekuwa wakikumbana na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na wazazi wao au walezi ambapo hivi sasa wanaonekana kuwa  waathirika wakubwa wa kuwatelekeza.
Moja ya tukio la kusikitisha ambalo liliwaliza  akina mama na watu wengine  walioshuhudia unyama  wa mama Enjoy turukale  kumpiga  mtoto wake wa kuzaa Teddy Turukale (2) kwa kutumia vitu vya ncha kali hadi kumvunja mguu.
Kisa na mkasa cha mama huyo kufanya unyama huo ni tabia ya mtoto huyo kukojoa na kunya mara kwa mara  kitendo kilichomkera na kuamua kumpa kipigo cha mbwa mwitu bila kujali ni mtoto ambaye ni malaika anayetenda jambo asilojua.
Mtoto Teddy  alifanyiwa ukatili na mama yake  mwanzoni mwa Januari mwaka huu akiwa nyumbani kwake Kisesa  jijini Mwanza kwa kupiga na kitu cha ncha kali eneo la paja.
Hata hivyo baada ya tukio hilo mama huyo aliamua kumpeleka Hospitali ya Rufaa Bugando na  kuombwa PF3  na madaktari ili aweze kutibiwa kitendo kilimchomfana mama huyo  amtoroshe hospitalini hapo na kumtekeleza kwa bibi yake Tereza Turikali eneo la Pasiasi.
Hata hivyo kutokana na mguu wa mtoto huo kuoza na kutoa harufu kali  kutokana na kutibiwa na mganga wa kienyeji akimuosha kwa dawa ya maji aina ya JIK, mguu uliendelea kuoza.
Kutokana na harufu kuenea mtaa mzima, majirani walianza kujiuliza maswali na hatimaye kubaini  kuna mtoto amefichwa ndani kwa bibi Tereza ambaye ni jirani yao na kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za Mtaa wa Pasiasi Juu, polisi na kituo cha kuokoa maisha ya watoto waliofanyiwa ukatili.
Kutokana na hali hiyo  MTANZANIA iliamua kuafutailia tukio hilo katika ngazi zote ili kujua hatma ya mtoto huyo baada ya kugundulika akiwa amefichwa  ndani ya nyumba ya bibi Tereza.
Akizungumza  na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Pasiasi Juu, Merry Joseph anasema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi wake aliwaita polisi na watumishi wa Kituo cha uokoaji watoto cha Foundation Karibu Tanzania (FKT) pamoja a polisi jamii na kuvamia nyumba hiyo.
Anasema kama mzazi alishindwa kuvumilia na kuanza kulia kutokana na jinsi mtoto alivyokuwa ameoza mguu huku ukiwa mweusi mithili ya mkaa (kama picha inavyoonekana).
Joseph anasema baada ya kumuokoa mtoto huyo walimkabidhi kwenye kituo cha FKT,  polisi kwa hatua zaidi ya matibabu na sheria.
Pamoja na mambo mengi lakini anasema kwamba ukatili dhidi ya watoto unaendelea kufanyika kutokana ugumu wa maisha na baadhi ya wazazi kutokuwa na elimu nzuri juu ya malezi na makuzi ndani ya familia zao.
Pia anasema asilimia kuwa ya wazazi wamekuwa wakiwafanyia ukatili watoto wao lakini hukimbilia kwa waganga wa kienyeji kuwatibu badala ya hospitali kw akuhofia kukamatwa.
MTANZANIA ilifanikiwa kufanya mahojiano na Mjumbe wa Mtaa huo, Juma  Fadhili, balozi wa shina 75 wa CCM, Mariam Twaha na polisi jamii wa mtaa huo, Joseph Sigareti ambao walifanikisha kufichukuliwa kwa mtoto huo ambapo walisema wamesikitishwa na unyama huo.
Kwa upande wa Mwezeshaji wa kituo cha FKT, Abimerick Richard anasema baada ya uvamizi ndani ya nyumba ya bibi  January  17 mwaka huu, siku ya pili yake walikabidhiwa mtoto huyo  na kumpaleka Hospitali ya Sekou Toure huku mguu ukiwa umeonza.
Anasema hata hivyo walishindwa kumtibu ndipo walipopelekwa Hospitali ya Sengerema DDH ambayo ina wataalamu  na kukatwa mguu Januari 19, 2014 na kukatwa mguu kama inavyoonekana kwenye picha.
Anasema kwamba hadi sasa mtoto huyo bado anaendelea na matibabu  na gharama zote wanatoa wao.
Katika suala la ukatili, anasema kwamba jamii  inachangia vitendo vya kinyama kuendelea kutokea kutokana na kuficha taarifa  na kuona jukumu hilo ni la Serikali pekee
Pia anaongeza kuwa vyombo vya dola vinachangia kwa kupindisha sheria hasa pale inapogundulika mwenye fedha au kigogo amefanya ukatili dhidi ya mtoto wake.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana hadi sasa linaendelea kuwasaka wazazi wa mtoto Teddy kwa kuwa hawajulikani walipo na bibi aliyekutwa na mtoto huyo anaendelea kuhojiwa.
 Naye Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Jalia Mtani anasema tafsiri ya ulinzi  ni kulinda kitu au kiumbe ili kisidhurike kwa namna yoyote ile.
Anasema kwa upande wa mtoto anapaswa kulindwa ili asiweze kunyanyaswa, kufanyiwa ukatili wa aina yoyote ile huku akitoa mifano kwamba sheria ya mtoto ya 2009 inakataza mtoto kutokwenda baa, kuagizwa sigara, kunywa pombe na ikibainika mzazi amekwenda naye katika mazingira hayo anatozwa faini ya Sh milioni moja hadi nne.
Mtani anasema kitendo cha watoto kuwapo mitaani ni sehemu ya ukatili unaosababishwa na wazazi kutokana na kutoelewaza au nyumba kukosa amani.
Anasema chanzo cha ukatili ndani ya familia ni usongo wa mawazo moyoni, hasiara, umasikini ambao unasababisha baadhi ya wazazi kutelekeza watoto na kuongeza kuwa familia isiyo na upendo lazima vitendo hivyo vitatokea.
Anasema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuacha vitendo hivyo na kufuata sheria zinavyoelekeza, hata hivyo aliongeza kuwa sheria zipo za kuadhibu mtoto kama amekosea.
Naye Padri wa Kanisa Katoliki la Nyarubere Jimbo la Geita Wilaya ya Nyanghwale, Thomas Kabika Mbilingi anasema vitendo vya ukatili ni unyama, mmomonyoko wa maadili, uvunjifu wa amri za Mungu, jamii, Serikali na jumuiya.
Padri Mbilingi anasema ukatili ni ukosefu wa upendo wa mtu kwa mtu, mtu kwa Mungu (Mathayo 7:12) inasema unayotaka kutendewa wewe watendee wenzako,  (Yohana 1:34) inasema amri mpya nawapeni ni agizo na fundisho la Yesu kwa ufuasi wake.
Anasema sababu za kutokea ukatili kwa watoto ni jamii au mtu binafsi asiye na upendo, maadili, utu lazima atatenda ukatili.Anaongeza kuwa Serikali, jamii kutokazia amri na  sheria kwa wananchi juu ya uhalifu na kusababisha ukatili kuongezeka.
Padri Mbilingi anasema ubinafsi unaonekana kutawala zaidi kuliko ujamaa ambao unaleta ukatili, pia anabainisha kwmaba watu wanaonekana kuacha dini ya mafundisho ya Yesu Kristo wa agano jipya na badale yake wanafuata agano la kale.
Anafafanua kwamba mafundisho ya agano la kale linaekeleza kuwa jina kwa jino yaani ukitendewa na mtu vibaya lipiza lakini agano jipya linafundisha kufuata maandiko ya Yesu ambaye anasema adui wako mpende.
Padri Mbilingi anasema ili kuzuia ukatili dhidi ya watoto lazima mafundisho na msisitizo ukaziwe popote kanisani, msikitini, mihadhara na kuongeza wahalifu wachukuliwe hatua.
Hata hivyo mwanasheria wa Kujitegemea , Abimerick Richard anasema sheria zilizopo hazitoi adhabu kali kwa wanaofanya ukatili wa watoto na kuitaka Serikali kuboresha sheria zake kwa kuongeza adhabu kali.
Kutokana na matukio ya ukatili  ni muhimu Serikali kuunganisha nguvu pamoja na taasisi zinazopinga vitendo hivyo zikiwamo Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN).

Mtandao wa Tecden ni  umoja wa watu na asasi ambao kwa pamoja wana nia ya kuunganisha sauti zao ili kuleta hamasa na mchango katika sera na programu zinazohusu malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo kwa kubadilishana habari, uzoefu na ufahamu katika malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo.

Kwa kuwa dira ya mtandao huo ni kuwa na ukakika wa taifa ambalo watoto wote tangu kutungwa mimba hadi miaka minane wanatunzwa na kulelewa vizuri kwa kupata haki za haki zao za msingi za kuishi na kukua vema .

Ni wakati muafaka sasa Serikali kuunganisha dhamira yake na kuunga mkono taasisi za namna hiyo katika kufanikisha ukatili nchini unakwisha.
Ikiwa Serikali itaungana  pamoja na FKT, Tecden na nyingine za namna hiyo, hakika watafanikisha kujenga mazingira bora ya kujengeana uwezo ili kuwezesha sera na  programu za maendeleo katika ngazi zote ili kuleta msukumo wa kuboresha huduma za maendeleo kwa watoto wadogo.
0683 608 958

MWISHO.

MAREKANI YALETA ELIMU YA KISASA TANZANIA



Marekani yaleta ukombozi sekta elimu ya kisasa Tanzania
*Sasa walimu wa sayansi kutoshika chaki
Na Benjamin Masese, Mwanza
MFUMO wa kisasa wa ufundishaji wa masomo ya sayansi bila mwalimu kushika chaki umezinduliwa nchini katika mikoa 10   kwa majaribio ya wanafunzi wa kidato cha pili.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi jijini Mwanza katika Shule ya Sekodari ya wavulana ya  Bwiru chini ya ufadhili wa taasisi kutoka  Marekani iitwayo  Opportunity Education Foundation inayojihusisha na masuala ya elimu.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa kwa walimu sita wa masomo ya sayansi na wanafunzi  162 wa kidato cha pili , Meneja Programu wa taasisi hiyo, Sadra Tetty alisema Marekani imemua kufanya majaribio Tanzania katika mikoa 10.

Tetty alisema vifaa vyenye mfumo huo vina mitaala yote inayofundishwa Tanzania na inaweza kubadilishwa kadri wizara ya elimu itakavyoona inafaa au kuongeza program nyingine.
Alisema kwa awamu ya kwanza wameanza katika majaribio ya mikoa kumi kwa  baadhi ya shule za sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha pili na ikiwa watafanikiwa katika mitihani yao wataendelea kufadhili mikoa mingine.
“Tumeamua kuwagawaia vifaa kila mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule tulizozichagua pamoja na walimu wote wa masomo ya sayansi ikiwa lengo ni kurahisha ufundishaji na kuboresha elimu pamoja na kukuza teknolojia.
“Shule tulizoanza kufanya majaribio juu ya mfumo huu zipo Dar es Salaam, Mwanza, Bukoba, Dodoma, Morogoro, Pemba, Rifiji, Arusha na Zanzibar.
“Ufadhili huu kwa Tanzania zimetengwa Dola milioni 10 za Marekani kwa majaribio na tutakuwa tunapita kukagua lakini matokeo yao ndio yatatoa mwelekeo sahihi kama unaeleweka au la,”alisema.
Tetty alisema mfumo huo umekuwa na mafanikio Marekani na hakuna mwalimu wa masomo ya sayansi anayeandika ubaoni na chaki, na kuongeza kuwa unaondoa utegemezi kati ya mwanafunzi na mwalimu katika kujifunza.
Alisema vifaa hivyo huchajiwa na umeme nyakati za usiku na kutumiwa mchana wakati wa masomo na kuwataka walimu wa masomo hayo kuvitumia kama vilivyokusudiwa sambamba na vile vya wanafunzi.

 Tetty alisema kuwa katika shule wanazofanyia majaribio tayari walimu wa masomo hayo wamekwisha pewa mafunzo.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Bwiru, Elias Kaboja alisema amefurahishwa shule yake kuwa katika majaribio ya mfumo huo na kuongeza kwmaba utarahisisha ufundishaji.
Alisema atahakikisha anawasimamia walimu wa masomo hayo kufanikisha kile kilicholengwa huku akiitaka Serikali kushirikiana na taasisi hiyo ili mfumo uenee nchi nzima.
Alisema anafurahishwa kuona kila mwalimu sita amepewa vifaa hivyo na wanafunzi 162 wa kidato cha pili wamepewa kila mmoja.
Alisema shule yake ina wanafunzi 780 na kati ya hao 162 ni kidato cha pili waliiopewa vifaa vya mfumo huo ambao utaanza kutumika Februari 3, mwaka huu.
Naye Mratibu wa Programu ya mfumo huo shuleni hapo, Iluminata Pascal ambaye pia ni mwalimu alisema uwepo wa vifaa hivyo utapunguza kazi ya uandaaji program ya kufundisha.
Hata hivyo moja ya changamoto iliyopo katika mfumo huo ni pale ambapo itatokea mabadiliko ya mitaala ya elimu kwani inalazimika kuingizwa katika vifaa hivyo.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo waliozungumza na MTANZANIA baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo walifurahishwa na ujio wa mfumo huo.
Miongoni mwa wanafunzi waliozungumza ni pamoja na Igunge Zakayo, Johnson Kaihuzi na Shaban Moshi ambao walisema wana shauku ya kutaka kuanza kuvitumia vifaa hivyo.

Wednesday 19 February 2014

WASOMI WANAPOFANYA UKATILI WA WATOTO WAO



Wasomi wapuuza sheria za watoto na kufanya ukatili
*Mtoto apoteza mikono kisa wizi wa viazi
Na   Benjamin Masese, Mwanza
MWAKA 2009 Serikali kupitia Bunge lake ilipitisha sheria za kuwalinda watoto ambayo ililenga kuweka usalama kwa watoto dhidi ya mazingira hatarishi na unyanyasaji.
Kwa mujibu wa sheria hiyo  inamtaka kila mtu kumtunza na kumlea mtoto katika maadili na makuzi mema bila kumfanyia ukatili wa aina yoyote ile.
Katika sensa iliyofanyika mwaka 2012 inaonyesha watanzania wote  ni zaidi ya  milioni  45 na kati ya hao asilimia 50 ni watoto ambao ni hazina ya taifa la kesho.
Katika sheria hizo za mtoto zimeanisha kanuni muhimu zikiwamo maslahi bora ya mtoto ambaye anapaswa kufanyiwa matendo mema ya msingi ya  kuishi bila ubaguzi, unyanyapaa kwa misingi ya jinsia, umri, asili yake, rangi, dini, hali ya kiafya, ulemavu, desturi, kabila, hali ya kiuchumi na nyinginezo kama hizo.
Sheria  hizo zinaelekeza kwamba  mtoto ana haki ya kuishi na wazazi, walezi na kukua katika mazingira ya amani kwa kupewa matunzo sahihi.
Pia sheria hiyo  inasema ni kosa kwa mlezi au mzazi wa mtoto kushindwa kutoa mahitaji ya msingi kwa ajili ya uhai na makuzi ya mtoto.
Inabainisha kwmaba kitendo cha mtoto kushindwa kupewa mahitaji ya msingi kinamtia hatiani mlezi au mzazi  kwa kutozwa faini  kuanzia Sh 500,000 hadi  Sh milioni au kifungu cha miezi sita hadi miaka mitatu.
Pamoja na uwepo wa sheria hizo lakini vitendo vya ukatili wa watoto wadogo umeendelea kufanyika nchini huku Kanda ya Ziwa ikionekana kuwa ni jambo la kawaidwa.
Ni jambo lisilo la kificho kwamba mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Mwanza, Mara, Shinyanga, Kagera, Simiyu na wilaya zake, vitendo vya ukatili kwa rika zote vimekuwa ni adhabu ya kawaida na   kuonekana ni haki kujeruhi, kuua au kumfanyia mtu ulemavu wa kudumu.
Mikoa hiyo hiyo imekuwa na historia ya vitendo vya ushirikina na  mauaji ya kikatili hali ambayo imebadilisha hadhi ya wakazi ndani ya taifa lao huku jamii nyingine ikiwaona  watu wa kuogopwa  na hatari kutokana na ukatili unaotendeka ndani ya maeneo yao.

“Ni hali ya kushangaza  kuona  wasomi tena waajiriwa wa Serikali katika sekta ya elimu na idara za kusimamia haki, usalama wa raia na mali zake wanakuwa sehemu  au miongoni mwa watu wanaotenda unyama wa kutisha kwa watoto wenye umri mdogo na kuwatelekeza bila matibabu yoyote”
Elfrida Nicholaus (7)  ni miongoni mwa watoto waliofanyiwa ukatili na mlezi wake  na mke wa mjomba wake, Ester Benedict Miti ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Sweya na kumficha ndani ya nyumba kwa siku bila matibabu”
Mtoto Elfrida alichomwa mikono na mwalimu Miti  mwaka jana  ambapo alimfunga  kitambaa na kumwagia mafuta ya taa kwa kile kilichodaiwa aliiba viazi vitamu kwa jirani yake.
Mtoto Elfrida alichukuliwa  na mjomba wake Selestine Kasendela ambaye ni  askari polisi wa kituo cha Kirumba Wilaya ya Ilemela  jijini Mwanza  kutoka kwa mama yake mzazi, Marina  Fabian anayeishi mkoani Kigoma.
Askari huyo alimchukua mtoto huyo kwa nia njema kwa lengo la kuja kukaa naye kwa kuwa mazingira aliyokuwa akiishi na mama yake mzazi  yalikuwa mabaya kutokana na kutengana na mme wake aliyemwachia watoto saba.
Hata hivyo mwalimu huyo baada ya kumfanyia ukatili huo  alimficha ndani bila matibabu huku akijitahidi kufanya siri ili majirani wasijue lakini mwisho wa siku waligungua baada ya kuwapo kwa harufu kutokana na vidole vya mikono kuoza na baadhi ya vingine kukatika.
Kitendo cha majirani kugundua tukio hilo kiliwafanya kutoa taarifa Kituo cha Polisi Igogo na kukamatwa lakini kutokana na mme wake kuwa askari hatua zozote hazikuweza kuchukuliwa.
Mtoto Elfrida alichukuliwa na kituo cha kuokoa watoto waliofanyiwa ukatili cha Foundation Karibu Tanzania (FKT) kwa ajili ya matibabu huku wakitarajia jeshi la polisi kuchukua hatua lakini mwisho wa siku hakuna hatua zilizochukuliwa  juu ya tukio hilo.
Hadi sasa tukio hilo halijafikishwa mahakamani kutokana na kile kinachodaiwa ni upelelezi unaendelea lakini ni dhahiri kuna hali ya kulindani
Kibaya zaidi wakati mtoto huyo anatibiwa  katika Hospitali ya Sengerema hadi aliporudishwa Mwanza kwenye kituo cha FKT, walezi hao yaani Mwalimu Miti na askari Kasendela hawakuweza kufika kumjulia hali au kumchukua .
Kitendo cha walezi hao ambao ni watumishi wa Serikali kumtekeleza mtoto huyo kimewafanya FKT kupelekea kesi Tume ya Haki za Binadamu Kanda ya Ziwa Februari Mwaka huu ili kuhakikisha haki inapatikana.
Kutokana na hali hiyo MTANZANIA ilitembelea kituo cha FKT kuona hali ya mtoto huyo pamoja na kufanya mahojiano na viongozi wa kituo hicho ambapo ilishuhudiwa watoto zaidi ya 25  waliofanyiwa ukatili akiwamo Elfrida  wakilelewa hapo.
Ndani ya kituo hicho, MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya watoto  wakiwa wamefanyiwa ukatili wa kuchomwa mikono, miguu, kichwa, tumbo, midomo , sehemu za siri,  kuchomwa kisu, kipigo sehemu mbalimbali  za miili yao kama picha zinavyoonekana.
Sababu zilizoelezwa na viongozi wa kituo hicho, ni kwamba watoto hao wamefanyiwa ukatili kutokana na kuiba fedha, kukojoa kitandani, kula mboga, tabia mbaya, uvivu, kuwa na kiburi na vitu vya namna hiyo.
Hakika kituo hicho kinaonekana wazi kuwa kimbilio la watoto wanaoteswa na wazazi na hata Serikali imekuwa ikichukua takwimu za mwaka watoto waliopokelewa hapo kwa kufanyiwa ukatili.
Akizungumza na MTANZANIA, Mratibu Mkuu wa FTK, David Othiambo anasema kwamba vitendo vya ukatili dhidi ya watoto hufanywa na wazazi wao lakini asilimia 90 hufanywa na mama mzazi.
Anasema kuwa kasi ya ukatili wa watoto wadogo unashika kasi Kanda ya Ziwa lakini kwa upande wa upande wa Jiji la Mwanza, Wilaya ya Nyamagana inaongoza kwani kwa wiki wanapokea watoto watatu hadi wanne waliofanyiwa ukatili wa kutisha.
Anasema kwa idadi hiyo kwa mwezi wanapokea watoto 16 ambapo kwa mwaka wanaokoa zaidi ya watoto 201 watoto  ambao wamefanyiwa ukatili wa namna mbalimbali.
Othiambo anasema kundi la watoto wanaofanyiwa ukatili ni kati ya umri siku moja hadi miaka 12 ambao ni waathirika wakubwa na kuongeza kwamba kituo kinapata shida kutokana na jamii kutokuwa tayari kutoa taarifa na kujua suala la kulinda haki za watoto ni la wote.
Anasema licha ya kuwapo na vyombo vya kisheria lakini bado havijafikia hatua ya kutenda haki hasa kwa wale viongozi na watu wenye fedha pale wanafanya ukatili dhidi ya watoto.
imefikia hatua ya wazazi kubaka watoto wao lakini kutokana na kutojua chombo cha kuwatetea wamekuwa wakibaki bila msaada wowote hadi pale anapojitokeza msamaria mwema kitoa taarifa.
Othiambo anasema asilimia 90 watoto alionao kituoni wamefanyiwa ukatili na wazazi wao kwa kupigwa na kuchomwa,  asilimia tatu wamepakwa na asilimia 7 wamenyanyaswa au kunyanyapaliwa.

0683608958
MWISHO.

VIONGOZI WA SERIKALI WANAPODIRIKI KUFANYA UBAGUZI OFISINI



Itikadi, ubaguzi wa RC Ndikilo Mwanza unahitaji dawa haraka
*Makada wa Chadema waanza kusakwa Serikalini
Na Benjamin Masese, Mwanza
WAKATI tunafikiria uhasama unaoendelea kati ya wafugaji na wakulima nchini kufikia hatua ya kuuana kama wanyama ,inaonekana wazi kuna baadhi ya viongozi wa Serikali wanafanya kazi kwa ubaguzi na itikadi za kisiasa.
Ni jambo la hatari kwa mustakabili wa taifa hili ikiwa hali hii itachukuliwa kirahisi ama kupuuzwa, kulindana kutokana na itikadi za vyama vya siasa au kwa maslahi binafsi.
Migogoro ya wafugaji na wakulima imeanza kitambo na wananchi  pamoja na wabunge hasa wa upinzani wamekuwa wakisema jambo hilo bungeni lakini Serikali imekuwa ikilichukulia ni propaganda zao za kujitafutia umaarufu.
Bila shaka maauji ya watu zaidi ya kumi yaliyotokea Wilaya ya Kiteto yamethihirisha na kuonyesha sura na uhalisia wa  kile kilichokuwa kikisemwa  mara kwa mara lakini kinachukuliwa poa.
Hakuna haja ya kuelezea kile kilichosemwa na Naibu Spika wa Bunge, Job Ndungai mbele ya Waziri Mkuu Pinda alipotembela wananchi wa Kiteto, kwa kuwa alisema wazi baadhi ya viongozi wa Serikali wanashiriki kwa namna moja katika mauaji hayo kwa manufaa yao binafsi.
Wakati tunatafakari ya wafugaji na wakulima lakini inaonekana kuna mkakati wa ubaguzi na chuki  unaendeshwa chini chini na viongozi  katika sehemu za kazi kwa kuangalia itikadi za vyama vya siasa, mkakati huu unaweza kuwa hatari kwa ustawi wa taifa.
Ni hali ya kustajabisha kuona Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evarist Ndikilo akifanya kazi kwa ubaguzi na chuki kutokana na itikadi za vyama vya siasa.
Ubaguzi  na chuki wa mkuu huyo ulidhihirika January 17 mwaka huu  wakati wa hafla iliyoandaliwa na Mamlaka ya Maji Safi na Taka Mwanza (MWAUWASA) ya kupokea hundi ya mkopo Sh milioni 300 kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (LAPF).
Fedha hizo zilitolewa na LAPF kwa ajili kukikopesha Chama cha Akiba na Mikopo cha Mamlaka ya Maji Safi na Taka Mwanza (MWAUWASA-SACCOS) ambacho imekuwa mkombozi wa watumishi wa mamlaka hiyo.
Katika hali ambayo haikutarajiwa wageni wa  LAPF waliokuwa wametoka Dodoma na watumishi wa Mwauwasa wakiwa tayari kumpokea mgeni rasmi ambaye ni Ndikilo, ilikuja taarifa kwa wote kwamba amepata dharura hivyo hatafika.
Kitendo hicho kiliwashangaza watu wengi  na kuhoji angemtuma hata mwakilishi wake kwa kuwa wageni walikuwa nje ya ukumbi wa Gand Hall kwa ajili ya mapokezi.
Macho ya wageni na waalikwa yalielekezwa kwenye ofisi ya Ndikilo ilipo kwa kuwa ni karibu kutoka eneo la hafla ilipokuwa ikifanyikia sawa na mita 95  huku kila mmoja akitafsiri ajuavyo juu ya kitendo hicho.
“Lakini wakati watu wakiondoka eneo hilo ilidokezwa  taarifa nyingine kwamba  Ndikilo hakuweza kufika kwa sababu Meneja  wa Saccos hiyo, Tungaraza Njugu  ni kada  na kiongozi mkubwa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) hivyo hawawezi kukaa meza moja”.
Ilifafanuliwa kwamba Meneja Njugu  ambaye ni Kiongozi wa Operesheni Kanda ya Ziwa Magharibi wa Chadema amekuwa akimtukana Ndikilo katika majukwaa na mikutano ya  kisiasa juu ya utendaji wake, hivyo upande mmoja kuwa na  chuki.
MTANZANIA ilifunga safari kwenda ofisi ya Saccos ya Mwauwasa ili kujua kwa kina hali hiyo ambayo viongozi ambao ni waajiriwa wa Serikali kufikia hatua ya kufanya kazi kwa chuki kutokana na itikadi za kisiasa.
Njugu anaanza kwa kusema anasikitishwa na kitendo kilichotokea na kuongeza kwamba imedhihirisha Ndikilo anaongoza Mkoa wa Mwanza kwa itikadi ya kichama na ubaguzi wa kisiasa.
Anasema haamini kama Ndikilo ametumwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) au ndio sera ya chama hicho  katika kuongoza  kwa ubaguzi wa watumishi kwa mlengo wa itikadi za kisiasa.
Njugu anasema taarifa ya Ndikilo kushindwa kufika eneo tukio kutokana na yeye kuwa kada wa Chadema ilielezwa na Zacharia Membo ambaye ni Afisa Utumishi Mwauwasa.
Anasema hali hiyo imempa wasiwasi juu ya usalama wake, ajira na mambo mengineya kifamiia  kwa kuwa Ndikilo ana nafasi ya kumtendea kitu chochote kwani ni mkuu wa mkoa na Mwenyekiti wa kamati  ulinzi na usalama.
Njugu anasema imedhihirisha wazi watumishi wa Serikali ambao ni makada wa Chadema wapo katika hali ya kubaguliwa na inaonyesha hawana haki ya kazi au kuajiriwa serikalini.
Anasema alipata nafasi ya  meneja wa Saccos hiyo kutokana na elimu na utalaamu wake, hivyo kuwa kada wa Chadema si dhambi na kuongeza kwamba kamwe  hafanyi kazi kwa itikadi za kisiasa.

Njugu anasema kuna kila sababu ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko ya nafasi hiyo ya ukuu wa mkoa kwani imedhihirisha chanzo cha madiwani watatu wa Chadema kufukuzwa ni nguvu yake inachangia.
“Sasa hivi Ndikilo namweka kama adui wangu namba moja katika maisha yangu, familia na ajira hivyo vyombo vya usalama nataka vijue hivyo nikipata tatizo lolote chanzo ni chuki za kisiasa za upande mmoja”.
Lakini anasema kutokana na ubaguzi huo na chuki wa Ndikilo haziwezi kuwa kikwazo katika kutekeleza majukumu yake ya kazi na kisiasa anakupokuwa nje ya Saccos.
Njugu anasema kwa nafasi yake hiyo hajawahi kufanya upendeleo wowote dhidi ya watumishi wa Mwauwasa na wengi wao wamejenga nyumba na kununua gari kupitia Saccos yao.
Inaonekana Ndikilo alikuwa na chuki dhidi ya mamlaka hiyo kwani aliwahi kulalamika mbele ya Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) juu ya tabia ya Mkurugenzi wa Mwauwasa, Anthony Sanga kushindwa kutoa taarifa kwake wakati Naibu Waziri wa Maji, Benilith Mahenge alipokuja Mwanza January 3 mwaka huu.
Ni kweli kabisa wakati Mahenge alipokuja kukabidhi vitendea kazi kwa halmashauri nne za Geita, Ukerewe, Sengerema na Nansio hakuwapo Mkuu wa mkoa wala askari yeyote kwa ajili ya ulinzi, hindicho ndicho kilimchomkasirisha na kuamua kumsema  Sanga mbele ya RCC.
Yamekuwapo na malalamiko dhidi ya Sanga kwamba ni miongoni mwa viongozi wababe, kiburi sawia na Ndikilo lakini wanaoumia kutokana na uhasama huo ni wananchi wanaohitaji huduma  za kijamii.
Mhandisi Sanga amekuwa akilalamikiwa na wananchi pamoja na waandishi wa habari Mkoa wa Mwanza juu ya kauli zake na hata kuwatishia maisha pale wanapokuwa wakimbana kutaka taarifa ya Mwauwasa kutokana na malalamiko ya wananchi.
Hata wanapojaribu kuandika maswali na kuyakabidhi kwake amekuwa akiyapuuza lakini wanapojaribu kuandika hali halisi ndipo ugomvi unapotokea na kutoa vitisho.
Mmoja wa watumishi wa Mwauwasa ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema ni dhahiri sasa kuna mkakati wa kumwondoa Njugu katika nafasi ya umeneja kwa kuwa elimu yake haikidhi viwango vya kusimamia saccos hiyo kwani imefikia kumiliki mabilioni ya fedha.
Ni wazi sasa  kumeibuka kasumba ya kutoelewana kati ya viongozi ngazi ya halmashauri, wilaya, mkoa na taasisi zake kutokana na itikadi za kisiasa na kusababisha kukwama kwa shughuli za maendeleo katika maeneo husika.
Itakumbukwa mwishoni mwa mwaka jana mpaka sasa kumekuwapo na migogoro kadha wa kadha maeneo mbalimbali  nchini kwa viongozi wa kulalamikiana huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuingilia majukumu ya mwenzake.
Pia kumekuwapo na hali ya kutofautiana kauli juu ya jambo moja  ambapo upande mmoja umekuwa ukidai kutenda haki huku mwingine ukilalamika.
Tumeshuhudia mkoani Arusha, mkuu wa mkoa huo akitofautiana kauli na Mkurugenzi wa jiji hilo juu ya wafanya biashara wadogo katikati ya jiji hilo na kusababisha madiwani kugawanyika katika pande mbili.
Ukiachia hilo kumekuwapo na mgogoro kati ya Meya wa Ilemela  na Mkuu wa wilaya mkoani Mwanza kwa kila mmoja kudai kuingilia majukumu ya mwingine.
Wimbi hilo linaonekana kuwagusa sana wakurugenzi wa Halmashauri kutofautiana na madiwani na watendaji wengi, kwa mfano Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Hassan Hidda amekuwa katika mgogoro na madiwani jambo ambalo linakwamisha maendeleo.
Hiyo ni mifano michache ambayo inaonesha kuna wimbi la viongozi walioaminiwa na kupewa dhamana ya kuwatumikia wananchi kushindwa kushirikiana na kuanza kutuhumiana.
Kwa tukio la RC Ndikilo la kutohudhuria katika hafla hiyo zikiwa zimesalia dakika kama kumi lilionesha sura mbaya kwa wageni waliotoka Dodoma kwa ajili kutoa mkopo kwa Mwauwasa, mpaka sasa haijulikani wageni hao walipewa majibu gani.
Ni vema sasa Rais Kikwete akawatazama watu wake kwa namna nyingine katika nafasi walizopewa kuziongoza kwa kuwa wanaelekea kuleta mgawanyiko ndani ya jamii moja na taifa moja vingine itafikia hatua ya wafugaji na wakulima.
0683608958
MWISHO.