Monday, 9 September 2013
UWEZO WA NAIBU SPIKA BUNGENI
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimesema uwezo wa Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai katika kuongoza Bunge unahatarisha amani, kuvunjika mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo sasa kutokana na kutokuwa na mtazamo mpana wa kufikiri.
Pia kimesema kuna ajenda ya chini chini inayoendelezwa na baadhi ya mawaziri, wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na kiti cha Spika katika kuhujumu malengo na nia ya Rais Kikwete kuwa na katiba mpya ifikapo 2015.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahimu Lipumba alisema kitendo cha Ndugai kuamuru polisi kumtoa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe ni cha aibu na kidikteta.
Profesa Lipumba alisema kuna baadhi ya viongozi Serikali (hawakuwataja) wanaojionesha wanamsaidia Rais Kikwete lakini ndani ya moyo wao wana ajenda za siri za kumhujumu.
Alisema kuwa viongozi hao wamekuwa wakitumia udhaifu wa Ndugai kwa kumshawishi kufanya kile wanachoona kinafaa kwa lengo la kukandamiza upinzania na kuhmhujumu Rais bila yeye kujua.
Alisema kuwa hivi Sasa Tanzania inakabiliwa na changamoto za matamshi hasi yanayotolewa na viongozi na asasi za Rwanda baada ya Rais Jakaya Kikwete kutoa ushauri wenye mantiki kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame kukutana na waasi wa kikundi FDRL kitendo ambacho kimeleta hali ya sintofahamu.
Pia alisema kuwa kitendo cha baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kufanya vikao vyao na kuitenga Tanzania huku wakizungumzia namna ya kuinua uchumi wao, kitendo ambacho kinamweka Rais Kikwete katika changamoto kubwa.
Alisema kuwa kitendo cha kiti cha Spika hasa kinapokaliwa na Ndugai kimekuwa kikiendesha Bunge kwa kupendelea Serikali kwa kadri kinavyoweza huku kikizima hoja za upinzani kwa makusudi.
“Kuna njama za wazi zinafanywa na kiti cha Spika kwa kutelekeza maoni ya wananchi na kupendelea ya Chama Cha Mapiunduzi (CCM), kwa upande wa Zanzibar hawakushirikishwa vizuri na hata wabunge wa CUF wanasema hawakushirikishwa.
“Moja ya njama za wazi ni ile ya wabunge 166 wa bunge la katiba wanaoipaswa kupendekezwa na taasisi mbalimbali na kuteuliwa na Rais, sisi CUF kinasikitishwa na mchakato unavyoendeshwa na jinsi uteuzi unavyopendekezwa.
“Hii katiba mpya itakuwa ni ya CCM sio ya Watanzania, na ombi la wabunge wa CUF ni kutaka muswada urudishwe kwa wananchi na kamati ijadili upya.
“ CUF inaendelea na juhudi za kuwasiliana na viongozi wa vyama vingine ili kuweka mkakati wa pamoja na kukabiliana na hujuma dhidi ya mchakato wa kupata katiba mpya na kuimarisha umoja wa kitaifa,”alisema.
Profesa Lipumba alisema kuwa kitendo cha Ndugai kumnyima nafasi Mbowe kinadhihirisha ni mpango mkakati wa kuminya hoja za upinzani na kutumia nguvu kumtoa nje ya Bunge hakikubaliki na amevunja sheria.
Profesa Ibrahimu alihoji kwamba angesimama Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, je asingepewa nafasi ya kusikilizwa na kuongeza kwamba baadhi ya Wabunge wa CUF akiwamo Mozza Abeid walivuliwa hijabu zao kitendo ambacho ni udhalilishaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment