Thursday, 20 February 2014

MTOTO AVUNJWA MGUU KISA ANAKOJOA KITANDANI



Ukatili  huu utaisha lini Kanda ya Ziwa?
*Mtoto avunjwa mguu kisa anakojoa ovyo

Na Benjamin Masese, Mwanza
ILE kauli ya kwamba ‘Uchungu wa mwana aujuaye mzazi’ inakosa uhalisia wake kutokana na  vitendo vya ukatili dhidi ya watoto kutokea maeneo mbalimbali ya nchi.
Sote tunafahamu watoto ambao ni tegemeo la  taifa la kesho wamekuwa wakikumbana na vitendo vya kinyama vinavyofanywa na wazazi wao au walezi ambapo hivi sasa wanaonekana kuwa  waathirika wakubwa wa kuwatelekeza.
Moja ya tukio la kusikitisha ambalo liliwaliza  akina mama na watu wengine  walioshuhudia unyama  wa mama Enjoy turukale  kumpiga  mtoto wake wa kuzaa Teddy Turukale (2) kwa kutumia vitu vya ncha kali hadi kumvunja mguu.
Kisa na mkasa cha mama huyo kufanya unyama huo ni tabia ya mtoto huyo kukojoa na kunya mara kwa mara  kitendo kilichomkera na kuamua kumpa kipigo cha mbwa mwitu bila kujali ni mtoto ambaye ni malaika anayetenda jambo asilojua.
Mtoto Teddy  alifanyiwa ukatili na mama yake  mwanzoni mwa Januari mwaka huu akiwa nyumbani kwake Kisesa  jijini Mwanza kwa kupiga na kitu cha ncha kali eneo la paja.
Hata hivyo baada ya tukio hilo mama huyo aliamua kumpeleka Hospitali ya Rufaa Bugando na  kuombwa PF3  na madaktari ili aweze kutibiwa kitendo kilimchomfana mama huyo  amtoroshe hospitalini hapo na kumtekeleza kwa bibi yake Tereza Turikali eneo la Pasiasi.
Hata hivyo kutokana na mguu wa mtoto huo kuoza na kutoa harufu kali  kutokana na kutibiwa na mganga wa kienyeji akimuosha kwa dawa ya maji aina ya JIK, mguu uliendelea kuoza.
Kutokana na harufu kuenea mtaa mzima, majirani walianza kujiuliza maswali na hatimaye kubaini  kuna mtoto amefichwa ndani kwa bibi Tereza ambaye ni jirani yao na kutoa taarifa kwa uongozi wa Serikali za Mtaa wa Pasiasi Juu, polisi na kituo cha kuokoa maisha ya watoto waliofanyiwa ukatili.
Kutokana na hali hiyo  MTANZANIA iliamua kuafutailia tukio hilo katika ngazi zote ili kujua hatma ya mtoto huyo baada ya kugundulika akiwa amefichwa  ndani ya nyumba ya bibi Tereza.
Akizungumza  na MTANZANIA, Mwenyekiti wa Serikali za Mtaa wa Pasiasi Juu, Merry Joseph anasema baada ya kupata taarifa kutoka kwa wananchi wake aliwaita polisi na watumishi wa Kituo cha uokoaji watoto cha Foundation Karibu Tanzania (FKT) pamoja a polisi jamii na kuvamia nyumba hiyo.
Anasema kama mzazi alishindwa kuvumilia na kuanza kulia kutokana na jinsi mtoto alivyokuwa ameoza mguu huku ukiwa mweusi mithili ya mkaa (kama picha inavyoonekana).
Joseph anasema baada ya kumuokoa mtoto huyo walimkabidhi kwenye kituo cha FKT,  polisi kwa hatua zaidi ya matibabu na sheria.
Pamoja na mambo mengi lakini anasema kwamba ukatili dhidi ya watoto unaendelea kufanyika kutokana ugumu wa maisha na baadhi ya wazazi kutokuwa na elimu nzuri juu ya malezi na makuzi ndani ya familia zao.
Pia anasema asilimia kuwa ya wazazi wamekuwa wakiwafanyia ukatili watoto wao lakini hukimbilia kwa waganga wa kienyeji kuwatibu badala ya hospitali kw akuhofia kukamatwa.
MTANZANIA ilifanikiwa kufanya mahojiano na Mjumbe wa Mtaa huo, Juma  Fadhili, balozi wa shina 75 wa CCM, Mariam Twaha na polisi jamii wa mtaa huo, Joseph Sigareti ambao walifanikisha kufichukuliwa kwa mtoto huo ambapo walisema wamesikitishwa na unyama huo.
Kwa upande wa Mwezeshaji wa kituo cha FKT, Abimerick Richard anasema baada ya uvamizi ndani ya nyumba ya bibi  January  17 mwaka huu, siku ya pili yake walikabidhiwa mtoto huyo  na kumpaleka Hospitali ya Sekou Toure huku mguu ukiwa umeonza.
Anasema hata hivyo walishindwa kumtibu ndipo walipopelekwa Hospitali ya Sengerema DDH ambayo ina wataalamu  na kukatwa mguu Januari 19, 2014 na kukatwa mguu kama inavyoonekana kwenye picha.
Anasema kwamba hadi sasa mtoto huyo bado anaendelea na matibabu  na gharama zote wanatoa wao.
Katika suala la ukatili, anasema kwamba jamii  inachangia vitendo vya kinyama kuendelea kutokea kutokana na kuficha taarifa  na kuona jukumu hilo ni la Serikali pekee
Pia anaongeza kuwa vyombo vya dola vinachangia kwa kupindisha sheria hasa pale inapogundulika mwenye fedha au kigogo amefanya ukatili dhidi ya mtoto wake.
Kwa upande wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana hadi sasa linaendelea kuwasaka wazazi wa mtoto Teddy kwa kuwa hawajulikani walipo na bibi aliyekutwa na mtoto huyo anaendelea kuhojiwa.
 Naye Afisa Ustawi wa Jamii Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Jalia Mtani anasema tafsiri ya ulinzi  ni kulinda kitu au kiumbe ili kisidhurike kwa namna yoyote ile.
Anasema kwa upande wa mtoto anapaswa kulindwa ili asiweze kunyanyaswa, kufanyiwa ukatili wa aina yoyote ile huku akitoa mifano kwamba sheria ya mtoto ya 2009 inakataza mtoto kutokwenda baa, kuagizwa sigara, kunywa pombe na ikibainika mzazi amekwenda naye katika mazingira hayo anatozwa faini ya Sh milioni moja hadi nne.
Mtani anasema kitendo cha watoto kuwapo mitaani ni sehemu ya ukatili unaosababishwa na wazazi kutokana na kutoelewaza au nyumba kukosa amani.
Anasema chanzo cha ukatili ndani ya familia ni usongo wa mawazo moyoni, hasiara, umasikini ambao unasababisha baadhi ya wazazi kutelekeza watoto na kuongeza kuwa familia isiyo na upendo lazima vitendo hivyo vitatokea.
Anasema Serikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuacha vitendo hivyo na kufuata sheria zinavyoelekeza, hata hivyo aliongeza kuwa sheria zipo za kuadhibu mtoto kama amekosea.
Naye Padri wa Kanisa Katoliki la Nyarubere Jimbo la Geita Wilaya ya Nyanghwale, Thomas Kabika Mbilingi anasema vitendo vya ukatili ni unyama, mmomonyoko wa maadili, uvunjifu wa amri za Mungu, jamii, Serikali na jumuiya.
Padri Mbilingi anasema ukatili ni ukosefu wa upendo wa mtu kwa mtu, mtu kwa Mungu (Mathayo 7:12) inasema unayotaka kutendewa wewe watendee wenzako,  (Yohana 1:34) inasema amri mpya nawapeni ni agizo na fundisho la Yesu kwa ufuasi wake.
Anasema sababu za kutokea ukatili kwa watoto ni jamii au mtu binafsi asiye na upendo, maadili, utu lazima atatenda ukatili.Anaongeza kuwa Serikali, jamii kutokazia amri na  sheria kwa wananchi juu ya uhalifu na kusababisha ukatili kuongezeka.
Padri Mbilingi anasema ubinafsi unaonekana kutawala zaidi kuliko ujamaa ambao unaleta ukatili, pia anabainisha kwmaba watu wanaonekana kuacha dini ya mafundisho ya Yesu Kristo wa agano jipya na badale yake wanafuata agano la kale.
Anafafanua kwamba mafundisho ya agano la kale linaekeleza kuwa jina kwa jino yaani ukitendewa na mtu vibaya lipiza lakini agano jipya linafundisha kufuata maandiko ya Yesu ambaye anasema adui wako mpende.
Padri Mbilingi anasema ili kuzuia ukatili dhidi ya watoto lazima mafundisho na msisitizo ukaziwe popote kanisani, msikitini, mihadhara na kuongeza wahalifu wachukuliwe hatua.
Hata hivyo mwanasheria wa Kujitegemea , Abimerick Richard anasema sheria zilizopo hazitoi adhabu kali kwa wanaofanya ukatili wa watoto na kuitaka Serikali kuboresha sheria zake kwa kuongeza adhabu kali.
Kutokana na matukio ya ukatili  ni muhimu Serikali kuunganisha nguvu pamoja na taasisi zinazopinga vitendo hivyo zikiwamo Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Watoto Wadogo Tanzania (TECDEN).

Mtandao wa Tecden ni  umoja wa watu na asasi ambao kwa pamoja wana nia ya kuunganisha sauti zao ili kuleta hamasa na mchango katika sera na programu zinazohusu malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo kwa kubadilishana habari, uzoefu na ufahamu katika malezi, makuzi na maendeleo ya watoto wadogo.

Kwa kuwa dira ya mtandao huo ni kuwa na ukakika wa taifa ambalo watoto wote tangu kutungwa mimba hadi miaka minane wanatunzwa na kulelewa vizuri kwa kupata haki za haki zao za msingi za kuishi na kukua vema .

Ni wakati muafaka sasa Serikali kuunganisha dhamira yake na kuunga mkono taasisi za namna hiyo katika kufanikisha ukatili nchini unakwisha.
Ikiwa Serikali itaungana  pamoja na FKT, Tecden na nyingine za namna hiyo, hakika watafanikisha kujenga mazingira bora ya kujengeana uwezo ili kuwezesha sera na  programu za maendeleo katika ngazi zote ili kuleta msukumo wa kuboresha huduma za maendeleo kwa watoto wadogo.
0683 608 958

MWISHO.

No comments:

Post a Comment