Thursday, 20 February 2014

MAREKANI YALETA ELIMU YA KISASA TANZANIA



Marekani yaleta ukombozi sekta elimu ya kisasa Tanzania
*Sasa walimu wa sayansi kutoshika chaki
Na Benjamin Masese, Mwanza
MFUMO wa kisasa wa ufundishaji wa masomo ya sayansi bila mwalimu kushika chaki umezinduliwa nchini katika mikoa 10   kwa majaribio ya wanafunzi wa kidato cha pili.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi jijini Mwanza katika Shule ya Sekodari ya wavulana ya  Bwiru chini ya ufadhili wa taasisi kutoka  Marekani iitwayo  Opportunity Education Foundation inayojihusisha na masuala ya elimu.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa kwa walimu sita wa masomo ya sayansi na wanafunzi  162 wa kidato cha pili , Meneja Programu wa taasisi hiyo, Sadra Tetty alisema Marekani imemua kufanya majaribio Tanzania katika mikoa 10.

Tetty alisema vifaa vyenye mfumo huo vina mitaala yote inayofundishwa Tanzania na inaweza kubadilishwa kadri wizara ya elimu itakavyoona inafaa au kuongeza program nyingine.
Alisema kwa awamu ya kwanza wameanza katika majaribio ya mikoa kumi kwa  baadhi ya shule za sekondari kwa wanafunzi wa kidato cha pili na ikiwa watafanikiwa katika mitihani yao wataendelea kufadhili mikoa mingine.
“Tumeamua kuwagawaia vifaa kila mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule tulizozichagua pamoja na walimu wote wa masomo ya sayansi ikiwa lengo ni kurahisha ufundishaji na kuboresha elimu pamoja na kukuza teknolojia.
“Shule tulizoanza kufanya majaribio juu ya mfumo huu zipo Dar es Salaam, Mwanza, Bukoba, Dodoma, Morogoro, Pemba, Rifiji, Arusha na Zanzibar.
“Ufadhili huu kwa Tanzania zimetengwa Dola milioni 10 za Marekani kwa majaribio na tutakuwa tunapita kukagua lakini matokeo yao ndio yatatoa mwelekeo sahihi kama unaeleweka au la,”alisema.
Tetty alisema mfumo huo umekuwa na mafanikio Marekani na hakuna mwalimu wa masomo ya sayansi anayeandika ubaoni na chaki, na kuongeza kuwa unaondoa utegemezi kati ya mwanafunzi na mwalimu katika kujifunza.
Alisema vifaa hivyo huchajiwa na umeme nyakati za usiku na kutumiwa mchana wakati wa masomo na kuwataka walimu wa masomo hayo kuvitumia kama vilivyokusudiwa sambamba na vile vya wanafunzi.

 Tetty alisema kuwa katika shule wanazofanyia majaribio tayari walimu wa masomo hayo wamekwisha pewa mafunzo.
Kwa upande wa Mkuu wa Shule ya Bwiru, Elias Kaboja alisema amefurahishwa shule yake kuwa katika majaribio ya mfumo huo na kuongeza kwmaba utarahisisha ufundishaji.
Alisema atahakikisha anawasimamia walimu wa masomo hayo kufanikisha kile kilicholengwa huku akiitaka Serikali kushirikiana na taasisi hiyo ili mfumo uenee nchi nzima.
Alisema anafurahishwa kuona kila mwalimu sita amepewa vifaa hivyo na wanafunzi 162 wa kidato cha pili wamepewa kila mmoja.
Alisema shule yake ina wanafunzi 780 na kati ya hao 162 ni kidato cha pili waliiopewa vifaa vya mfumo huo ambao utaanza kutumika Februari 3, mwaka huu.
Naye Mratibu wa Programu ya mfumo huo shuleni hapo, Iluminata Pascal ambaye pia ni mwalimu alisema uwepo wa vifaa hivyo utapunguza kazi ya uandaaji program ya kufundisha.
Hata hivyo moja ya changamoto iliyopo katika mfumo huo ni pale ambapo itatokea mabadiliko ya mitaala ya elimu kwani inalazimika kuingizwa katika vifaa hivyo.
Baadhi ya wanafunzi wa kidato cha pili wa shule hiyo waliozungumza na MTANZANIA baada ya kukabidhiwa vifaa hivyo walifurahishwa na ujio wa mfumo huo.
Miongoni mwa wanafunzi waliozungumza ni pamoja na Igunge Zakayo, Johnson Kaihuzi na Shaban Moshi ambao walisema wana shauku ya kutaka kuanza kuvitumia vifaa hivyo.

No comments:

Post a Comment