Wasomi wapuuza sheria za watoto na
kufanya ukatili
*Mtoto apoteza mikono kisa wizi wa
viazi
Na Benjamin Masese, Mwanza
MWAKA 2009
Serikali kupitia Bunge lake ilipitisha sheria za kuwalinda watoto ambayo
ililenga kuweka usalama kwa watoto dhidi ya mazingira hatarishi na unyanyasaji.
Kwa mujibu
wa sheria hiyo inamtaka kila mtu
kumtunza na kumlea mtoto katika maadili na makuzi mema bila kumfanyia ukatili
wa aina yoyote ile.
Katika sensa
iliyofanyika mwaka 2012 inaonyesha watanzania wote ni zaidi ya
milioni 45 na kati ya hao
asilimia 50 ni watoto ambao ni hazina ya taifa la kesho.
Katika
sheria hizo za mtoto zimeanisha kanuni muhimu zikiwamo maslahi bora ya mtoto
ambaye anapaswa kufanyiwa matendo mema ya msingi ya kuishi bila ubaguzi, unyanyapaa kwa misingi
ya jinsia, umri, asili yake, rangi, dini, hali ya kiafya, ulemavu, desturi,
kabila, hali ya kiuchumi na nyinginezo kama hizo.
Sheria hizo zinaelekeza kwamba mtoto ana haki ya kuishi na wazazi, walezi na
kukua katika mazingira ya amani kwa kupewa matunzo sahihi.
Pia sheria
hiyo inasema ni kosa kwa mlezi au mzazi
wa mtoto kushindwa kutoa mahitaji ya msingi kwa ajili ya uhai na makuzi ya
mtoto.
Inabainisha
kwmaba kitendo cha mtoto kushindwa kupewa mahitaji ya msingi kinamtia hatiani
mlezi au mzazi kwa kutozwa faini kuanzia Sh 500,000 hadi Sh milioni au kifungu cha miezi sita hadi
miaka mitatu.
Pamoja na
uwepo wa sheria hizo lakini vitendo vya ukatili wa watoto wadogo umeendelea
kufanyika nchini huku Kanda ya Ziwa ikionekana kuwa ni jambo la kawaidwa.
Ni jambo
lisilo la kificho kwamba mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwamo Mwanza, Mara,
Shinyanga, Kagera, Simiyu na wilaya zake, vitendo vya ukatili kwa rika zote
vimekuwa ni adhabu ya kawaida na kuonekana ni haki kujeruhi, kuua au kumfanyia mtu
ulemavu wa kudumu.
Mikoa hiyo
hiyo imekuwa na historia ya vitendo vya ushirikina na mauaji ya kikatili hali ambayo imebadilisha
hadhi ya wakazi ndani ya taifa lao huku jamii nyingine ikiwaona watu wa kuogopwa na hatari kutokana na ukatili unaotendeka
ndani ya maeneo yao.
“Ni hali ya kushangaza kuona wasomi tena waajiriwa wa Serikali katika sekta
ya elimu na idara za kusimamia haki, usalama wa raia na mali zake wanakuwa
sehemu au miongoni mwa watu wanaotenda
unyama wa kutisha kwa watoto wenye umri mdogo na kuwatelekeza bila matibabu
yoyote”
“ Elfrida Nicholaus (7) ni miongoni mwa watoto waliofanyiwa ukatili
na mlezi wake na mke wa mjomba wake,
Ester Benedict Miti ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Sweya na kumficha
ndani ya nyumba kwa siku bila matibabu”
Mtoto Elfrida
alichomwa mikono na mwalimu Miti mwaka
jana ambapo alimfunga kitambaa na kumwagia mafuta ya taa kwa kile
kilichodaiwa aliiba viazi vitamu kwa jirani yake.
Mtoto
Elfrida alichukuliwa na mjomba wake Selestine
Kasendela ambaye ni askari polisi wa kituo
cha Kirumba Wilaya ya Ilemela jijini
Mwanza kutoka kwa mama yake mzazi,
Marina Fabian anayeishi mkoani Kigoma.
Askari huyo
alimchukua mtoto huyo kwa nia njema kwa lengo la kuja kukaa naye kwa kuwa
mazingira aliyokuwa akiishi na mama yake mzazi yalikuwa mabaya kutokana na kutengana na mme
wake aliyemwachia watoto saba.
Hata hivyo
mwalimu huyo baada ya kumfanyia ukatili huo alimficha ndani bila matibabu huku akijitahidi
kufanya siri ili majirani wasijue lakini mwisho wa siku waligungua baada ya kuwapo
kwa harufu kutokana na vidole vya mikono kuoza na baadhi ya vingine kukatika.
Kitendo cha
majirani kugundua tukio hilo kiliwafanya kutoa taarifa Kituo cha Polisi Igogo
na kukamatwa lakini kutokana na mme wake kuwa askari hatua zozote hazikuweza
kuchukuliwa.
Mtoto
Elfrida alichukuliwa na kituo cha kuokoa watoto waliofanyiwa ukatili cha
Foundation Karibu Tanzania (FKT) kwa ajili ya matibabu huku wakitarajia jeshi
la polisi kuchukua hatua lakini mwisho wa siku hakuna hatua
zilizochukuliwa juu ya tukio hilo.
Hadi sasa
tukio hilo halijafikishwa mahakamani kutokana na kile kinachodaiwa ni upelelezi
unaendelea lakini ni dhahiri kuna hali ya kulindani
Kibaya zaidi
wakati mtoto huyo anatibiwa katika
Hospitali ya Sengerema hadi aliporudishwa Mwanza kwenye kituo cha FKT, walezi
hao yaani Mwalimu Miti na askari Kasendela hawakuweza kufika kumjulia hali au
kumchukua .
Kitendo cha
walezi hao ambao ni watumishi wa Serikali kumtekeleza mtoto huyo kimewafanya
FKT kupelekea kesi Tume ya Haki za Binadamu Kanda ya Ziwa Februari Mwaka huu
ili kuhakikisha haki inapatikana.
Kutokana na
hali hiyo MTANZANIA ilitembelea kituo cha FKT kuona hali ya mtoto huyo pamoja
na kufanya mahojiano na viongozi wa kituo hicho ambapo ilishuhudiwa watoto
zaidi ya 25 waliofanyiwa ukatili akiwamo
Elfrida wakilelewa hapo.
Ndani ya
kituo hicho, MTANZANIA ilishuhudia baadhi ya watoto wakiwa wamefanyiwa ukatili wa kuchomwa
mikono, miguu, kichwa, tumbo, midomo , sehemu za siri, kuchomwa kisu, kipigo sehemu mbalimbali za miili yao kama picha zinavyoonekana.
Sababu
zilizoelezwa na viongozi wa kituo hicho, ni kwamba watoto hao wamefanyiwa
ukatili kutokana na kuiba fedha, kukojoa kitandani, kula mboga, tabia mbaya,
uvivu, kuwa na kiburi na vitu vya namna hiyo.
Hakika kituo
hicho kinaonekana wazi kuwa kimbilio la watoto wanaoteswa na wazazi na hata
Serikali imekuwa ikichukua takwimu za mwaka watoto waliopokelewa hapo kwa
kufanyiwa ukatili.
Akizungumza
na MTANZANIA, Mratibu Mkuu wa FTK, David Othiambo anasema kwamba vitendo vya
ukatili dhidi ya watoto hufanywa na wazazi wao lakini asilimia 90 hufanywa na
mama mzazi.
Anasema kuwa
kasi ya ukatili wa watoto wadogo unashika kasi Kanda ya Ziwa lakini kwa upande
wa upande wa Jiji la Mwanza, Wilaya ya Nyamagana inaongoza kwani kwa wiki wanapokea
watoto watatu hadi wanne waliofanyiwa ukatili wa kutisha.
Anasema kwa
idadi hiyo kwa mwezi wanapokea watoto 16 ambapo kwa mwaka wanaokoa zaidi ya
watoto 201 watoto ambao wamefanyiwa
ukatili wa namna mbalimbali.
Othiambo
anasema kundi la watoto wanaofanyiwa ukatili ni kati ya umri siku moja hadi
miaka 12 ambao ni waathirika wakubwa na kuongeza kwamba kituo kinapata shida
kutokana na jamii kutokuwa tayari kutoa taarifa na kujua suala la kulinda haki
za watoto ni la wote.
Anasema
licha ya kuwapo na vyombo vya kisheria lakini bado havijafikia hatua ya kutenda
haki hasa kwa wale viongozi na watu wenye fedha pale wanafanya ukatili dhidi ya
watoto.
imefikia
hatua ya wazazi kubaka watoto wao lakini kutokana na kutojua chombo cha
kuwatetea wamekuwa wakibaki bila msaada wowote hadi pale anapojitokeza msamaria
mwema kitoa taarifa.
Othiambo
anasema asilimia 90 watoto alionao kituoni wamefanyiwa ukatili na wazazi wao
kwa kupigwa na kuchomwa, asilimia tatu
wamepakwa na asilimia 7 wamenyanyaswa au kunyanyapaliwa.
0683608958
MWISHO.
No comments:
Post a Comment