Sunday 25 August 2013

BOMBA LA GESI KUTANDAZWA LEO.26/8/2013



Bomba la gesi ya Mtwara kutandazwa leo
Na Benjamin Masese, aliyekuwa Lindi
BOMBA la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam, linaanza kutandazwa leo likianzia mkoani Lindi.
Kutokana na hali hiyo, Serikali imeonya kwamba, yeyote atakayethubutu kuharibu miundombinu ya bomba hilo, atachukuliwa hatua.
Taarifa hiyo ilitolewa juzi na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alipofanya ziara ya kukagua, ubora wa vifaa, rasilimali watu na  maandalizi ya miundombinu ya kutandaza bomba hilo.
Wakati wa ziara hiyo ya siku moja, alikuwapo pia Balozi wa China nchini, Lu Youging, viongozi mbalimbali wa Serikali na viongozi wa kampuni zinazotandaza bomba hilo.
Profesa Muhongo alisema ameridhishwa na maandalizi yanavyokwenda, kwa kuwa kuna vifaa vya kisasa na imara.
Kesho kutwa (leo), utandazaji wa bomba unaanza rasmi na kwa maandalizi niliyoshuhudia, nina imani mradi huu utakamilika kabla ya Desemba mwaka 2014.
“Naomba Watanzania wawe na imani kubwa na watoe ushirikiano kwani utandazaji wa bomba utafanyika katika pande zote mbili, kwa maana ya nchi kavu na baharini.
“Mradi huu ni wa gharama kubwa na kama mnakumbuka, tulikopa fedha kutoka Benki ya Exim ambazo ni Dola za Marekani bilioni 1.2 kwa masharti nafuu.
“Pamoja na kwamba nia yetu ni nzuri, kuna baadhi ya watu wasiopenda maendeleo ya nchi hii, nataka kuwahakikishia Watanzania wote, kwamba usalama wa miundombinu hii utakuwa shwari na kama mtu anataka kushughulikiwa na Serikali, basi ajaribu kuihujumu atakiona cha mtema kuni.
“Hapa tumeshuhudia Watanzania 45 walioanza kupata ajira kama madereva, vibarua, kampuni za usafirishaji, huu ni mwanzo tu na ikifika sehemu ya kuhitaji watu wenye utaalamu, wataajiriwa wenye utaalamu,” alisema Profesa Muhongo.
Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, mabomba yanayotandazwa ni ya aina mbili yakiwamo ya inchi 36 na uzito wa tani tano na yenye inchi 24 yakiwa na tani tatu ambayo alisema kwa ujumla wake yatadumu kwa miaka 30 na kama yakitunzwa vizuri yatadumu hadi miaka 70.
“Tunataka ifikapo mwaka 2016, tuwe na umeme wa megawati 3000 na mwingine wa ziada wa utakaokuwa ukiuzwa nje ya nchi ikiwamo Kenya ambayo imeleta maombi ya kuuziwa megawati 1000,” alisema.
Pamoja na kufanya ziara hiyo juzi, Profesa Muhongo alisema itakuwa ni endelevu na itakuwa ikihusisha waandishi wa habari.
Naye, Balozi Youging, alisema gesi ni kitega uchumi kizuri ambacho kinaweza kuwaondoa Watanzania katika umasikini.
“China ni moja ya nchi iliyonufaika na gesi na ndio maana raia wake ni wataalamu wa nishati hiyo, naamini upatikanaji wa gesi hapa Tanzania, utasaidia Watanzania kuondokana na matumizi ya mkaa na kuni.
Kwa upande wake, Meneja Mradi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, Mhandisi Baltazari Thomas, alisema hadi sasa watu 163 wamepata  ajira katika awamu ya kwanza na kati ya hao Watanzania ni 68.
 Mwisho.
Rufaa dhidi ya Zombe kusikilizwa leo
Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
MAOMBI ya Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP) ya kuongezewa muda wa kukata rufaa dhidi ya aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam, Abdallah Zombe na askari wenzake wanane walioachiwa huru katika shtaka la mauaji, yanatarajiwa kusikilizwa leo.
Maombi hayo yanatarajiwa kusikilizwa katika Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji Aloyisius Mujuluzi.
Katika shauri hili, DPP aliwasilisha maombi ya kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa, baada ya Mahakama ya Rufaa ya Tanzania, kutupilia mbali rufaa ya awali kwa sababu ilikuwa na makosa ya kisheria.
Rufaa hiyo ilitupwa baada ya kubaini kuwapo kwa dosari katika hati ya kusudio la kukata rufaa na mahakama kukataa kuamuru makosa yaliyojitokeza yafanyiwe marekebisho.
“Kusudio la kukata rufaa ndio linatengeneza rufaa yenyewe, kwa kuwa kuna makosa, hakuna rufaa iliyopo mahakamani, kama makosa yangejitokeza katika rufaa yenyewe, Mahakama ingeweza kutoa maelekezo ya kufanyiwa marekebisho, rufaa inatupwa, Jamhuri ina haki ya kuwasilisha rufaa nyingine nje ya muda, baada ya kuomba kufanya hivyo,” alisema Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Watatu, Edward Rutakangwa.

Majaji wengine waliokuwa wakisikiliza rufaa hiyo kabla ya kutupwa ni Jaji Mbarouk Mbarouk na Bethuel Mmila ambao awali walipoketi kwa ajili ya kuanza kusikiliza rufaa iliyokatwa na DPP kupinga hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, ziliibuka hoja za dosari katika hati ya kusudio la kukata rufaa.

Zombe na wenzake walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini wakazi wa Mahenge Morogoro pamoja na dereva teksi mmoja.

Kabla ya jopo la mawakili wa Serikali lililokuwa linamwakilisha DPP ambao ni Mawakili wa Serikali Wakuu, Edwin Kakolaki, Vitalis Timon, Prudence Rweyongeza na Mawakili Revocatus Mtaki na Alexander Mzikila, halijaanza kuwasilisha hoja zao za kukata rufani, Jaji Mbaraouk alilihoji jopo hilo kuhusu dosari hiyo.

“Mahakama inataka kujiridhisha juu ya kinachosomeka katika hati ya kusudio la kukata rufaa, ambayo inasema mnapinga hukumu iliyotolewa na Jaji Massati wa Mahakama ya Rufaa. Sasa hii inakuja kwetu kama marejeo au mapitio," alihoji Jaji Mbarouk.

Hata hivyo, Wakili Timon, alikiri kuhusu dosari hiyo na hivyo kuiomba Mahakama kuwaruhusu kufanya marekebisho na kisha kuendelea kusikiliza rufaa hiyo.

Jaji Rutakangwa alihoji upande wa Jamhuri kuwa hati hiyo ina dosari, kwa kuwa inaonyesha wanakata rufaa kupinga hukumu ya Jaji wa Mahakama ya Rufaa, wakati hajawahi kukaa kusikiliza shauri hilo kwa kuwa si sahihi.

Ombi la mawakili wa Serikali la kuomba kufanyia marekebisho hati hiyo, lilipingwa vikali na mawakili wanaowawakilisha Zombe na wenzake ambao ni Richard Rweyongeza, Majura Magafu na Dennis Msafiri.

Katika shauri hili, mbali na Zombe, wajibu rufani wengine ni polisi Christopher Bageni, Ahmed Makele, Jane Andrew, Koplo Emmanuel Mabula, Michael Shonza, Abeneth Saro, Rajabu Bakari na Festus Gwasab.

Serikali ilikata rufaa hiyo kupinga hukumu iliyotolewa Agosti 17, 2008 na Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.

 mwisho.


Nyavu haramu za Sh milioni 150 zateketezwa

Na Ahmed Makongo, Bunda

NYAVU haramu 3,280 zenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 150, zimekamatwa wilayani Bunda, mkoani Mara na kuteketezwa kwa moto.

Nyavu hizo ziliteketezwa jana kwa usimamizi wa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Joshua Mirumbe.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo, Mirumbe alisema kuwa nyavu hizo ambazo ni pamoja na makokolo ya kuvulia sangara, nyavu zenye matundu madogo, timba na makokolo ya dagaa, zimekamatwa na vyombo vya dola kutokana na msako unaoendelea wilayani hapa.

Alisema kuwa msako huo unashirikisha askari wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), polisi, mgambo pamoja na maofisa wa idara ya uvuvi.

Alisema operesheni hiyo aliianzisha mwenyewe na kwamba itakuwa endelevu kwa kuwa lengo lake ni kutokomeza wavuvi haramu wilayani hapa.
Ili kuhakikisha uvuvi haramu unakomeshwa wilayani hapa, aliwataka viongozi wa Serikali za vijiji, kata na Vikundi vya Ulinzi wa Rasilimali za Ziwa Victoria (BMU), kuhakikisha wavuvi haramu wanakamatwa.

Alisema kama uvuvi haramu utaendelea katika baadhi ya maeneo, kitakachofuata ni kukamatwa kwa viongozi wa maeneo utakakokuwa ukifanyika uvuvi huo.

“Hatua ifuatayo ni kukamata viongozi wa Serikali za vijiji na kata na wale wa BMU ambao tutakuta kwenye maeneo yao kunaendeshwa shughuli za uvuvi haramu,” alisema Mirumbe.

Aliwaonya viongozi hao kutojihusisha na shughuli za uvuvi haramu, kwa kuwa inasemekana baadhi yao wanafadhili wavuvi hao.

Naye, Ofisa Uvuvi wa Wilaya ya Bunda, Stephen Ochieng, alisema nyavu hizo zilikamatwa katika Tarafa za Kenkombo na Nansimo ambako ndiko uvuvi haramu ulikoota mizizi.

Aliongeza kwamba, wapo wavuvi haramu ambao wamekuwa wakitumia sumu na kwamba uvuvi huo unahatarisha afya za wananchi pamoja na kuua viumbe hai wa majini.

Aidha alitumia fursa hiyo kuwaomba viongozi wa wilaya jirani zilizoko kwenye ziwa Victoria, kudhibiti wavuvi haramu, kwani unapofanyika msako katika Wilaya ya Bunda, baadhi ya wavuvi hao hukimbilia katika wilaya hizo.

Mwisho.






No comments:

Post a Comment