Tuesday 13 August 2013

UKATILI HUU MPAKA LINI TANZANIA?


Mama akipigwa na mume wake baada ya kutofautina
Baba akimdhibiti mke wake kwa kumkata mapanga baada ya kuona ngumi, mateke na fimbo havikutosha
 
Na Benjamin Masese, Dar es Salaam

UKATILI wa kijinsia ni jambo kubwa kwenye ajenda za haki  za binadamu kimataifa.Ukatili unaweza kuwapata wanaume na wanawake lakini mara nyingi wanawake na watoto ndio waathirika wakubwa.

Hali hii imetokana  na mifumo mbalimbali iliyopo na uhusiano wa kijinsia ulivyo katika jamii zetu hapa nchini ambapo kundo moja hujiona ni bora kuliko kundi lingine.

Kwa miaka mingi wanaume wamechukuliwa kuwa katika daraja la juu kuliko mwanamke nah ii imejionyesha na kuendelea kuonekana wazi katika  nyanja zote za kijamii, kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi.

Mazoea hayo yamejengwa tangu zamani huku kukiwa na ngazi za kifamilia hadi kitaifa jambo ambalo ni hatari katika jamii nyingi Barani Afrika na sehemu nyingine duniani.

Kutokana na hali hiyoilivyo mpaka sasa, kuna haja kubwa ya kutoa elimu juu ya ukatili katika jamii zetu hususani vijijini kunakotokea kila siku vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake.

Bila Serikali, taasisi, mashirika na wadau wengine wanapaswa kuungana pamoja na ili kuwaelimisha jamii juu ya kupambana na kuzuia ukatili wa kijinsia ili kuleta mabadiliko katika jamii.

Sote tunatambua kwamba ukatili ni kitendo chochote anachofanyiwa binadamu na kumsababishia maumivu au athari kimwili, kiakili au kisaikolojia.Kumekuwapo na vitendo vya ukatili vingi tena vya kukusudia, kulazimisha, kutisha au kugofya dhidi ya wanawake kutaka kufanya jambo au tendo la ngono bila hiari yao.

Binadamu yeyote anaweza kufanyiwa ukatili wa aina tano  ukitegemea  na utamaduni na historia  ya jamii husika. Mara nyingi ukatili huo hufanyika kati ya wanandoa wa wapenzi lakini wanawake mara nyingi wamekuwa wakisumbuliwa zaidi na ukatili wa kijinsia katika uhusianohuo.

Moja ya ukatili ni ule wa kimwili ambao mtu hufanyiwa kitendo ambacho kinaumiza mwili na madhara yake huonekana moja kwa moja  na wakati mwingine mtendewa ukatili anaweza kuhisi maumivu bila mtu mwingine kutambua kuwa amefanyiwa ukatili wa kimwili.

Baadhi ya mifano ya ukatili wa kimwili ni pamoja na vipigo, shambulio la kimwili, kuchomwa moto, matumizi ya silaha, kuvutwa nywele, kusukuma, kunyonga mkono au mguu, kupigwa kichwani na kuchomwa na kitu chenye ncha kali sehemu yoyote ya mwili.

Pia  upo ukatili wa kisaikolojia ambao mtu anatendewa  na unamsababishia maumivu kiakili, kihisia huku mtenda kutotambua mwenzake anaathirika, mfano matusi kwa njia ya maneno au ishara yenye lengo la kudhalilisha, vitisho na kutishia kufanya fujo, maneno ya kufehedhesha, kudharau, kutishia kutoa siri, kuingiliwa faragha, kutishiwa kuuawa na mengine mengi.

Vile vile kuna ukatili wa uhusiano wa kingono ambao huambatana  na vitendo vinavyohusiana na masuala ya ngono, kwa mfano unyanyasaji wa kijinsia, kujamiiana kwa maharimu, ubakaji ndani ya ndoa, ulawiti, utekaji na usafirishaji  wa wanawake au wanaume na watoto kwa ajili ya ngono na vitendo vingine vya namna hiyo.

Upo ukatili wa kiuchumi ambao humnyima fursa za kiuchumi mwanamke au mwanaume katika kujiongezea kipato na kuchangia katika maendeleo.Aina  hiyo ya ukatili huwapata wanawake kutokana na hali yao ya kuwa tegemezi kwa wenzi wao.

Kitendo cha wanawake kuwa tegemezi kwa wanaume kimekua kinawaathiri sana kwani wanakosa kauli katika mali za familia na kutoshirikishwa kwenye maamuzi ya maendeleo.

Pia kuna ukatili unaotokana na tamaduni au mila potofu zetu hapa nchini ambazo zinakinzani na haki za binadamu jambo linalochangia kuwapo kwa vitendo vya ukatili. Baadhi ya ukatili wa mila potofu ni pamoja na ndoa za kushurutisha za utotoni, kutakasa wajane, kurithi wajane, utekeaji, matambiko ya kingono kwa watoto, miiko ya chakula na ukatili utokanao na mahari.

Kutokana na  uendelezaji wa vitendo vya ukatili nchini, kituo cha Msaada wa Sheria  kwa Wanawake Tanzania (WLAC)  kimeamua kuanzisha kampeni ya kupinga vitendo hivyo na kutoa msaada wa kisheria kwa wanawake  ili kuleta usawa  wa kijinsia Tanzania.

Taasisi ya WLAC  ni shirika lisilo la Serikali lililoanzishwa mwaka 1994 chini ya sheria ya makampuni sura ya 212 na pia limekuwa likiendeleza shughuli  za kitengo cha msaada wa sheria  SUWATA kilichoanzishwa mwaka 1989.

Kati ya madhumuni ya WLAC ni kutoa msaada wa sheria ju ya masuala yanayowakabili wanawake kama ndoa, mirathi, mikataba, biashara, ajira, uwakilishi mahakamani na huduma nyingine zinazofanana na hizo.

Pia imekuwa katika harakati za kujenga mtandao wa mashirika pamoja na taasisi zenye mwelekeo unaofanana na WLAC na kuratibu kwa pamoja shughuli za uhamasishaji umma kuhusu haki za wanawake na watoto.

Si jambo la kificho kwani wanawake wamekuwa katika changamoto kubwa hasa pale wanapokuwa katika ajira rasmi na hata zisizokuwa rasmi, baadhi yao wamekuwa  wakikosa nafasi za kufanya kazi mahali walipoomba kazi auhata katika ngazi ya familia kutokanana sababu mbalimbali.

Katika maeneo ya kazi, uzoefu unaonyesha wazi kuna kazi za wanawake na kazi za wanawake, wanawake waliobahatika kupata ajira wengi utawakuta nafsi za chini zaidi kama mapokezi, uhudumu wa ofisi, kazi za usafi na katibu mukhatsi.

Wakati mwingine baadhi ya wanawake wamelazimika kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na wakuu wao wa kazi ili kupata mahitaji yao.Wanawake wa namna hiyo huishia kwenye migogoro na waume zao au wapenzi wan a hatimaye uhusiano huo huharibika kabisa na kufukuzwa kazi.

Kazi zinazohitaji mwanamke kusafiri sana, kufanya kazi muda mrefu, wakati wa usikuau zinazohusisha kukutana na watu mbalimbali mara nyingi zimesababisha migogoro katika ndoa.

Hata hivyo wanawake wengi wamekosa fursa ya kujishughulisha ili kuongeza pato la familia, ambapo kwa wale waliobahatika kupata ajira zisizo rasmi wengi wao wanaishi kwa masharti na kutokuwa huru na wanapata mapato yanatokanayo nakazi wanayofanya.

Suala la ukatili lina upana wake ambapo upo ukatili wa kijinsia unaotokana na lugha ambapo maneno mbalimbali yamekuwa yakitumika kumwelezea mwanamke ambayo uhalisia wake ni ukatili wa kijinsia.

Maneno hayo yamekuwa yakitolewa katika kuelezea maumbile na tabia ya baadhi ya wanawake, matumizi ya lugha hiyo kwa sehemu kubwa huchangia kuonyesha mfumo dume ambao ndio unaotawala maisha ya watu ya kila siku. Matumizi ya lugha yanadhihirisha dhana potofu kwamba kundi la wanaume lina nguvu na ni bora kuliko wanawake.

Asilimia kubwa na mazoea yaliyopo sasa ni kwamba neno mwanamke amekuwa akichukuliwa ni kama chombo cha kumstarehesha mwanaume, mfano kuna maneno ya kama changundoa, sahani ya babu, namba nane, twiga na mengine kam hayo ambayo huonesha kuwa mwanamke ni dhaifu kuliko mwanaume.

Maneno mengine yanayoendana na hayo wakati mwingine yanaweza kutolewa dhidi ya wanaume, kwa mfano bushoke, dume la mbegu lakini yote yameelekzwa kwa wanawake kumuonyesha mwanaume ni bora.

Hata hivyo upo ukatili katika vyombo vya habari na matangazo ya kibiashara, mfumo wa habari na utoaji wa habari zenyewe umekuwa ukionesha taswira ya mwanamke kama chombo cha kumburudisha mwanaume, mfano matangazo, picha na mziki hutumiwa  na kuonyesha  wanawake kama sehemu ya matangazo ya biashara.




Kutokana na hali hiyo hivi karibuni WLAC kupitia wanasheria wake waliandaa semina iliyohusisha  wanawake na wanaume  wanaojiita wanabadiliko kutoka mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na kutoa elimu juu ya mambo kadhaa ya ukatili wa kijinsia nchini unaotokea katika nyanja mbalimbali ndani ya jamii.

Wanasheria wa WLAC waliokuwa wanatoa elimu kwa wanabadiliko ni pamoja na Lilian Lwanga na Hildegard Msina ambao walitoa ushahidi jinsi wanawake wanavyoteseka ndani ya ndoa zao pamoja na kunyang’anywa urithi wa mme wake mara anapofariki na kuacha familia.

Kwa upande Lwanga alibainisha kwamba katika utafiti walioufanya katika kadhaa nchini wamebaini asilimia 75 ya wananawake walio ndani ya ndoa hawana uhuru wa kijitawala katika maisha yao ya kila siku kutokana na kufanyiwa vitendo vya ukatili na wenzi wao.

Pia anasema walibaini wanaume wengi vijijini wamekuwa wakivunja ndoa zao au kuwatelekeza wake wao baada ya kujifungua watoto wenye vichwa vikubwa, midomo ya sungura na wengine wa namna ambapo aliitaka Serikali kuchukuliwa hatua za kisheria ili kukomesha hali ya ubaguzi, unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake.


WLAC imeamua kuendesha kampeni maalum ijulikanayo kwa jina la TUNAWEZA kwa wanamabadiliko ili kupinga vitendo vya ukatili na unyanyasaji nchini ambavyo vinaonekanakuwa jambo la kawaida katika  jinsia ya kike.

 Lwanga anasema msaada wa kisheria unaotolewa na WLAC umekuwa na mafanikio makubwa  kwani umeweza kuwasaidia wanawake kwa kuwawakilisha makahamani hadi  kurudishiwa nyumba walizokuwa wamenyang’anywa na ndugu wa marehemu kama urithi.

Anasema katika utafti wao mikoani wamebaini wanawake bado wananyanyaswa, wanapigwa na waume  lakini  hawako tayari kuwasema kwenye vyombo vya dola na kuongeza wameshuhudia ndoa nyingi zimevunjika kwa sababu ya mtoto kuzaliwa na kichwa kikubwa au mdomo wa wazi yaani wa sungura.

Lwanga anasema tatizo la watoto kukimbilia mjini na kuwa kuombaomba linatokana na ndoa kuvunjika, elimu ndogo kwa akina mama ya kutojua sheria zinazowapa haki yao, umasikini na mila potofu.

Anasema asilimia kubwa ya wananchi hasa wa vijini wanaishi kwa kuzingatia mila zao, hawajui  mabadiliko yaliyopo, wananyanyaswa kwa njia ya ngono, kiuchumi, kishambulio na kisaikolojia lakini hawajui namna ya kujisaidia kisheria kwani tangu awali Serikali haijaweka misingi ya kuwalinda wananwake na kuwapa uhuru.

Pamoja na mambo mengi ya unyanyasaji wa wanawake, Lwanga anaitaka Serikali kuacha mazoea ya kutegemea asasi, mashirika na ufadhili wa mataifa makubwa ya nje kuja nchini kutatua matatizo yanayowakabili wananchi wake badala yake inapaswa kupeleka elimu vijijini hususani katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.


Lwanga anasema kwamba ukatili unaofanywa dhidi ya wanawake nchini hauwezi kuvumiliwa ambapo anawataka  wanawake kuwafikisha wanaume kwenye vyombo vya dola aple wanapotendewa vitendo vya unyanyasaji.

Anasema binadamu yeyote anapofanyiwa ukatili  humsababishia kuwa na maumivu au athari kimwili, kiakili na kisaikolojia ambapo mwanamke anapofanyiwa ukatili huo athari kubwa kuliko mwanaume.

Anasema hivi sasa WLAC kwa kushirikiana na wakuu wa utekelezaji wa kampeni ya TUNAWEZA  wamedhamiria  kufikisha elimu ya ukatili wa kijinsia kwa watu 1,600,000 ifikapo mwaka 2013 ikiwa lengo ni kupunguza vitendo hivyo kwa wanawake ambavyo vimeonekana ndani ya jamii ni vitu vya kawaida.

Lwanga anasema madhumuni ya WLAC ni kutoa msaada wa sheria juu ya masuala yanayowakabili wanawake kama ndoa, mirathi, mikataba, kusimamia kesi mahakamani, kuendesha semina, ziara za mafunzo na kuhamasisha umma kuhusu haki za wanawake na watoto.

Pamoja na mambo mengi , wanasheria wa WLAC waliahidi kuendelea kutoa msaada wa kisheria mikaoni bure kwa wanawake na watoto ikiwa lengo ni kuleta usawa wa kijinsia Tanzania.

Hivyo sasa wakati umefika kwa Seriakli kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha vitendo vya unyanyasaji kijinsia vinakomeshwa haraka, pia vitendo vilivyoibuka hivi karibuni vya mateka kwa watu wanaopigania haki zao havipaswi kufumbiwa macho.

Tunapaswa kutambua kwamba katika hali halisi binadamu wote wamezaliwa huru huru na wote ni sawa mbele ya sheria hivyo hakuna mwenye haki ya kumfanyia mwenziwe ukatili wa aina  yoyote.

Vitendo hivi vinapofanyika ni kinyume cha sheria na mikataba mbalimbali ya haki za binadamu ambayo Tanzania imekuwa ikiisaini ili kushirikiana na mataifa makubwa kupambana na vitendo hivyo, sasa ni mwito kwa serikali kutekeleza mikataba hiyo kwa vitendo na sio maneno tupu. Maoni benjaminmasese@yahoo.com, 0655/0769-688300


MWISHOOO  





3 comments:

  1. Replies
    1. Haya kaka naona mambo yako, NASHUKURU SANA KWA KUNIONA NA KUSOMA BLOG YANGU

      Delete