Thursday 15 August 2013

LWAKATARE HOI

Polisi, Dk. Slaa jino kwa jino

Na Benjamin Masese, Dar es Salaam

WAKATI Jeshi la Polisi likiendelea kumng’ang’ania  Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA), Wilfred Lwakatare kwa tuhuma za kupanga njama za kudhuru watu, imedaiwa kuwa afya ya kiongozi huyo imezidi kudhoofika.



Lwakatare ambaye alikamatwa Machi 13, 2013 makao makuu ya chama hicho  na maofisa watatu wa polisi na kuwekwa rumande hadi sasa  kwa mahojiano imeelezwa kwamba afya yake imezidi kuzorota kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao.
Hata hivyo siku mbili  baada ya kushikiliwa Lwakatare alianza kulalamika kwa  wakili wake, Nyaronyo Kichere kwamba hajisikii vizuri kutokana na ugonjwa wa kisukari alionao huku akishindwa kula chakula inavyotakiwa.
Kutokana na hali, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Wilbrod Slaa jana  aling’aka na kusema Jeshi la Polisi lijipange kwa lolote litakalotokea kwa Lwakatare ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za afya yake.
Akizungumza na MTANZANIA jana kwa njia ya simu alisema anashangazwa na kitendo cha polisi kushindwa kutoa  ushirikiano na mawakili wa Lwakatare  pamoja na viongozi wa CHADEMA jambo ambalo linaleta wasiwasi mpango uliopo dhidi ya kiongozi huyo.

“Mwandishi unachotaka kujua juu ya Lwakatare ni kweli lakini binafsi nashindwa  nikueleze nini kwa sababu polisi hawataki kushirikiana na mawakili wala sisi viongozi.

“Hapa nilipo sina taarifa yoyote kutoka kwa mawakili wa Lwakatare kwa sababu hiyo hiyo ya kutokuwapo na ushirikiano na polisi, sasa kwa hali hiyo naomba ifahamike kwamba  chochote kitakachotokea kwa kiongozi wetu wanapaswa kujibu polisi.

“Sijui polisi wana mpango gani na Lwakatare kwani vitendo anavyofanyiwa haviendani na tuhuma zake, itakumbukwa siku moja baada ya kukamatwa tulipeleka chakula polisi hawakutaka kukipokea.

“Kama ambavyo hawatoi ushirikiano kwa vyombo vya habari pia nasi hata simu hawapokei,  kwa upande wa chama tunashindwa cha kuwaambia naombeni muwabane polisi wawaeleze kinachoendelea na walichopanga kesho (leo),”alisema.

Alipoulizwa kama chama kina mpango gani kutokana na afya ya Lwakatare kuendelea kuzorota rumande huku polisi wakikataa kutoa ushirikiano  wa karibu, alisema kwa kuwa suala hilo lipo kwenye vyombo vya sheria wanawaachia mawakili na wanasheria wao.
Hivi karibuni Wakili wa Lwakatare anukuliwa na vyombo vya habari alidai kuwa mteja wake ameshindwa kula chakula inavyotakiwa kutokana  ugonjwa wa kisukari alionao.

Kichere alisema mteja wake anatembea kwa kujivuta kitendo kinachomtia hofu kutokana na hali halisi  aliyomwona nayo na kuongeza kwamba anahangaika sana  kuhakikisha  anapata dhamana lakini  haoni matunda

“Mteja wangu ni mgonjwa wa kisukari, kwa kawaida hutakiwa kula chakula na kunywa maji mengi, lakini nimehangaika sana, leo (jana) nilikuwa na matumaini kwamba atapelekwa mahakamani ambapo nilijipanga kwa kuandaa watu makini wenye hati za nyumba nikiwa na imani kwamba angepata dhamana, lakini wamemrudisha mahabusu,” alisema Kicheere.

MTANZANIA ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova kuzungumzia hilo simu yake iliita bila kupokewa.
Alipotafutwa kwa mara nyingene na muda tofauti simu yake iliita na kuzimwa pia alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ hakuweza kujibu chochote.
Jana baadhi ya  vyombo vya habari viliripoti kwamba leo Kova anatarajiwa kuwataja majina ya watuhumiwa waliohusika kumteka na kumjeruhi Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda.

Pamoja na hilo ilielezwa kwamba polisi wanamshikilia mtu mmoja aliyetambulika kwa jina  la Joseph Ludovick akihusihwa na tukio la kigaidi.
Ilielezwa kwamba Ludovick alikamatwa  na makachero wa polisi mkoani Iringa baada ya kupatikana kwa taarifa zinazomhusisha kushiriki kupanga njama za  kudhuru watu.
Ludovick  anahusishwa katika tukio la kutekwa na kujeruhiwa  kibanda kutokana na mazingira halisi lilivyotokea tukio hilo.

Mwisho.


No comments:

Post a Comment