Monday 12 August 2013

SERENGETI ILIVYOVAMIWA VIJIJI VYAKE



HISTORIA YA WANGOREME

Na Benjamin Masese, Dar es Salaam
MKOA  wa Mara ni miongoni mikoa ya Tanzania Bara ambapo  mji wa Musoma  ndipo makaoa makuu ya mkoa huo.
Mara imepakana na mikoa ya Mwanza na Shinyanga  upande wa Kusini, Arusha upande wa Kusini-Mashariki, Kagera  upande wa Magharibi mwa Ziwa  Nyanza au Viktoria na Kenya upande wa mashariki.
Idadi ya wakazi ni zaidi ya milioni mbili na makabila ni mengi kuliko mikoa yote ya Tanzania ispokuwa Jiji la Dar es Salaam.
Baadhi ya makabila yaliyopo Mkoa wa Mara ni wajaruo, wajita, waruri, wazanaki, wakabwa, wakiroba, wasimbati, wangoreme, wakwaya, waikoma, wanata, waisenye, waikizu, wasizaki, wasukuma, wataturu ne mengine wengi.

Kuna wilaya ya saba ambazo ni Bunda, Serengeti, Tarime, Rorya, Butiama, Musoma Mjini na Musoma Vijijini.
Katika makala ya leo nitazungumzia kabila wa Wangoreme wanaoishi Wilaya ya Serengeti. Wangoreme wametokea Carogos nchini Ghana miaka mingi iliyopita.
Kabila la Wangoreme na Waikoma  mzazi wao ni mmoja aliyejulikana kwa jina la Sabayaya Wandira ambaye ni miongoni mwa msafara wa mtandao uliokuwa ukitoka Misri kupitia Somalia hadi Kenye ambapo waliingilia Mto Mara na kuweka makazi yao Serengeti.
Msafara mwingine wa kabila wa Wangoreme iliingia Serengeti kupitia njia ya Mkoa wa Manyara na baadhi yao kuweka makazi yao hapo.
Vijiji vya kabila la Wangoreme vilivyoitengeneza Wilaya ya Serengeti  ni Mugumu,Ikorongo, Borenga, Nyiboko, Buchanchari, Nyansurumunti, Mto Mara (Ghitende), Wigero, Baranga, Sirori Simba, Remng’orori , Mikomariro.
Vingine ni Mto Msamo-Tirina, Manchemwero, Nyankomogo, Issenye, Rigicha, Wegete, Nata, Rubana na kuunganisha tena Mugumu ambapo ndipo makao Makuu ya Wilaya ya Serengeti.

Lakini Vijiji hivyo vimevamiwa  na kabila la Wakurya wenye asili koo ya waasi kwa upande Magharibi, upande wa Kusini pamevamiwa na Waikizu na Waisenye na upande wa Magharibi wamevamia wakurya halisi kutoka Kenye na Tarime.
Pamoja na uvamizi huo lakini kabila la Wangoreme wameungana na kabila la Waikizu, Wanata na Waisenye na kuwa kitu kimoja tofauti na Wakurya wenye tabia tofauti ya ukatili na wizi wa mifugo.
Miiko ya Wangoreme

Mtu aliyeua mwenzake- Kabila la Wangoreme wamekuwa na miiko yao kulingana na tukio lenyewe, kwa mfano mtu aliyeua mwenzake ukiachia masuala ya kisheria, mara nyingi ukoo wa pande zote mbili hukaa na kukubaliana fidia ambayo ni idadi ya ng’ombe kuanzia saba na mbuzi au kondoo saba.
Baada ya fidia hiyo hufanyika matambiko fulani ambayo huashiria kusameheana  na kushiriki kula chakula pamoja.
Mwanamke aliyeshindwa kujifungua- Mwanamke aliyeshindwa kujifungua mtoto akiwa ndani ya ndoa au nje ya ndoa (ukiacha masuala ya kiafya), mara nyingi huadhibiwa kwa kupakwa majivu kama mchawi.
Mbali ya majivu hayo hunyolewa nywele kwa kutumia aidha chupa, wembe,mkasi na kisu huku akikatwa au kung’atwa kichwani  na kufanyiwa vidonda vya makusudi, pia huanza kufanya kazi kabla ya kupona.
Kuoa-Katika suala la kuoa au kuolewa mara nyingi wazazi wa kijana  ndio wanaochagua binti wa kuoa wakati upande wa binti wazazi hufuatilia historia ya jina na wazazi wao kama wana sifa ya kuwa ndugu wa kuoana.
Idadi halisi wanawake wa kuona ni kuanzia wawili hadi wadi wanne inategemea utajiri wa mtu mwenyewe na wingi wa shughuli zake.
Baada ya kuoana, marafiki wa pande zote mbili walisiosimamia ndoa hiyo hufanyiwa matambiko ya kupakwa mafuta ya ng’ombe usomi  ikiwa ni laana ya kutoibiana wala  kutembea na mke wa mwenzie.
 Mahali za kuoa mwanamke enzi za mababu zetu ilikuwa ni ng’ombe 80-60, enzi za baba zetu 50-30 lakini hadi sasa  20-6 ambapo thamani ya ng’ombe mmoja sasa ni Sh 300,000- 500,000.
 Wanawake kuoana ‘nyumba ntobhu’
Suala la wanawake kuoana ni jambo ambalo linafanywa na Kabila la Wangoreme na Wakurya, hii hufanyika pale aidha mwanamke anapojifungua watoto wote wa kike na kuolewa wote.
Pia hutokea pale mwana mke anapokuwa ndani ya ndoa lakini haukufanikiwa kupata mtoto  hata mmoja ambapo hulazimika kuoa mke mwenzake na kumpa uhuru wa kuzaa na mtu yeyote au kumchagulia mwanaume ndani ya familia au ukoo wake.
Lengo kuu la mke kuoa mke mwenzake ni kupata mtoto wa kiume ili kuendeleza ukoo wake na kusimamia mali zake alizonazo.

Hukumu ya Wangoreme-Ukiweka pembeni sheria, hukumu kubwa ya Wangoremaikiwa umefanya kosa kisha unakana  kukusanywa vitu vinavyoaminiwa ni hatari kwa afya yako na kulazimishwa kuviruka, pia kuna fuvu la kichwa cha binadamu ‘ekehore’ ambalo huwekwa maji machafu ya nguo zako na kunyweshwa.
Kukeketwa/kutahiriwa-Enzi za mababu wetu kijana au binti kutahiriwa-kukeketwa ni miaka 18-25 kwa kutumia kisu na wembe lakini kutokan na mabadiliko ya teknolojia jinsia ya kike imepigwa marufuku.
Pamoja na kupigwa marufuku bado ukeketaji unaendelea kwa jinsia ya kike na vitendo hivyo hufanyika kati ya umri mwaka mmoja hadi mitano kwani imani ni kupunguza hamu ya kujamiliana. Pia Wangoreme wanaamini kuoa mwanamke ambaye hajakekeketwa ni kuleta mkosi au haramu nyumbani.
Mapigano ya ukoo-Awali kulikuwa na mapigano ya koo na koo ambapo yalimalizwa kabisa kwa kuanzisha utaratibu kubadilisha watoto katika pande mbili jambo hilo husimamiwa na mabalozi wa nyumba kumi.
Ni kwamba kama mwanamke amejifungua watoto zaidi ya watatu anachukuliwa na kukabidhiwa koo nyingine hivyo upande wa pili kitendo ambacho kimewafanya kuwa kitu kimoja yaani ndugu wa damu.
Chakula,ufugaji-Asili ya Wangoreme ni wafugaji wa wanyama aina ya ng’ombe, mbuzi, kondoo, kuku na ndege aina ya kuku, bata, njiwa ambapo viumbe hivyo hutumika kama kitoweo, kitega uchumi.
Pia mazao yanayolimwa na Wangoreme ni mahindi, mtama, mihogo, viazi vitamu, maboga, ulezi ambapo zao kuu la  biashara ni pamba, ufuta, karanga  na Tumbaku.

Mboga halisi ya Wangoreme ni majani ya kunde,maharage, mlenda, msusa, mchicha na wakati wa kubadilisha au kuwapo kwa mgeni ni dagaa, nyama, samaki  na vitoweo vingine.
Masharti katika Chakula.
Miiko ya wangoreme ni kwamba wamefanya mgawanyo katika suala la nyama, kwanza vijana wametengewa kula kidali, wanawake wametengewa kula shingo, bibi miguu na baba na wazee wengine moyo na mgongo.
Ikibainika mmoja amekula sehemu ya nyama ya kundi fulani inaweza kuleta ugomvi mkubwa na hata aliyekula atakwenda kuinunua dukani na atashitakiwa kwenye vikao vya familia.

Mgeni wa heshima anapotembela rafiki yake anachinjwa mbuzi, ng’ombe au kuku lakini moja ya sharti ni kwamba kama amechinjiwa yeye lazima ale filigisi na asipoiona mezani atasusa kula.
Nguo- Asili ya nguo za kabila la Wangoreme enzi hizo zilikuwa ni ngozi za wanyama hasa mbuzi na swala  ambapo zilikuwa zinaambwa na kuondolewa nywele zote na aliyeruhusiwa kuzivaa ni kijana mwenye umri miaka 18 na kuendelea lakini baada ya nguo kuja walianza kuvaa hadi leo.
Silaha-Silaha kubwa  ya kabila la Wangoreme ni upinde na mikuki ambapo mafunzo ya kutumia zana hizo hufanyika wakati wa jando.
Ili kuhakikisha umekuwa hodari na mtaalamu wa silaha hizo lazima vijana hao wanaagizwa hifadhini kuwainda wanayama na kuleta nyama nyumbani.
Msiba,wizi- Wakati wa msiba, watu wote wa jirani na ndugu hujumuika pamoja kushiriki mazishi.
 Lakini mzee anapofariki asiyekuwa na mali mara nyingi anazikwa kama alivyozaliwa na ili kuepusha kuzikwa hivyo huwa na utaratibu wa kuweka mtoto wake wa kike rehani kwa mtu mwenye uwezo ili ampe ng’ombe ya kushughulikia msiba.
Mtoto anapokuwa mkubwa ataolewa na kijana wa yule aliyetoa msaada kwa familia ya marehemu aidha kwa kuongeza mahali nyingine au ile ya awali inategemea na wakati uliopo.
Kwa upande wizi unapotokea ndani ya kabila la Wangoreme lazima itapigwa baragumu ikiashiria hatari na watu wote huondoka nyumbani na upinde, mikuki  wakiwa tayari kwa lolote.
Nyumba, Vitanda-Nyumba za asili za Kabila la Wangoreme ni msonge ambazo zinajengwa na miti lakini kwa upende wa mwezekaji nyasi hutafutwa mtaalamu ili kuzuia maji ya mvua yasiingie ndani.
Kwa upande wa vitanda vya asili ni kuunganishs miti kwa mfani wa kitanda cha kisasa lakini panapotakiwa kuweka change inaambwa ngozi ya ng’ombe.
Nyimbo
Pia nyimbo zao za asili ni zeze na ngoma aina ya mbegete, kinanda, lukana ambapo zinapopigwa huchezeshwa mabega huku wanawake  na wanaume husogeleana kwa kukusana vifua.
Maoni -O769 688300 
================

MIPAKA YA VIJIJI ITATUGHARIMU BAADAYE

 


Mapigano ya mipaka ya majimbo yazuka Mara
*RC aizuia tume ya wizara
*Asema ilienda kinyemela
*Wassira, Dk. Kebwe wanena
*Mipaka yang’olewa
*Wananchi waahidi kumwaga damu

Na Benjamin Masese, Dar es Salaam
MAJIMBO  matatu ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mara yameingia katika mvutano  mkali wa kugombea mipaka yao  huku dalili za wazi za wananchi kushika mapanga, mishale na upinde zikianza kuonekana.
Mipaka hiyo ni  ile inayotenganisha Wilaya ya Musoma Vijijini, Serengeti, Bunda  ambayo inahusisha vijiji vya Sirori Simba(Musoma Vijijini), Remng’orori (Serengeti) na Mekomariro (Bunda).
Mgogoro wa mipaka hiyo ulianza kuibuika kwa mara ya kwanza mwaka 1978 lakini  hakuna suluhisho lililopatikana licha ya mikutano kadhaa kufanyika ikiwahusisha viongozi ngazi ya mkoa.

Waliovamia maeneo ya mipaka hiyo ni  wafugaji, wakulima huku wakianza kuweka makazi ya kudumu na shughuli za kijamii ambapo pande zote  zikidai yuko Wilaya yake.
Dalili za kuanza mapigano hayo zilianza kuonekana mwanzoni mwa mwezi huu baada ya wananchi wa Wilaya ya Musoma Vijijini kung’oa mabango  ambapo wananchi wa Wilaya ya Bunda wao wakichimba mitaro na kuweka alama za mipaka inayowatenganisha  na Wilaya ya Serengeti na Bunda huku wakitoleana vitisho.
DC Serengeti
Akizungumza na MTANZANIA juzi kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Joshua  Mirumbe alikiri kuwapo na mgogoro huo huku akisema kuwa umeanza kushughulikiwa na ngazi zote.
“Ni kweli upo mgogoro huo naohusisha wilaya tatu lakini kutokana na uzito wa suala hilo tayari tume imetoka Makao Makuu ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuja kushughulikia mipaka hiyo.
“Hivi tunavyozungumza viongozi ngazi ya mkoa, wilaya, kata, tarafa, vijiji wanashirikiana pamoja kuhakikisha kila mmoja anapata haki yake bila kuingia katika mapigano,”alisema kwa ufupi.

RC Mara
Akizungumza jana kwa njia simu, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Gabriel Tupa alikiri kuwapo na mgogoro huo huku akiwaomba wananchi kutoingia kwenye mapigano ya wao kwa wao kwa kuwa athari yake ni kubwa.
“Mgogoro huu ni mkubwa na ndio maana watalaam kutoka makao makuu ya Wizara ya Ardhi wameletwa ikiwa lengo ni kupata suluhisho lisilopendelea upande mmoja.
“Hasira za wananchi zilitokana na watalaam hao kwenda kwa wananchi bila kuwa na wakuu wa wilaya zote tatu huku wakitumia jina langu kwamba nimewaagiza.
“Kwa kweli walikosea na ndio maana nimewasimamisha kwanza na kuwaagiza wakuu wa wilaya wazungumze nao kwa kuwapa elimu na kuwashauri watoe ushirikiano ili wote kwa pamoja tupate suluhisho la kudumu.
“Kikubwa ninachosema  ni kwamba uamuzi wa mgogoro huu upo mikononi mwao lakini kama wamejiandaa  na mapiganoya mikuki, mishale na mapanga ni kuongeza tatizo.
“Nawasihi watoe ushirikiano kwa kuwa kamati zote zitaundwa  na wao ambapo watatoa historia yote ya mipaka kwa tume ya wizara ili kupata taswira halisi, pia nawaomba wananchi kuwa na subira hadi tume itakapokamilisha kazi yake,”alisema.
Mwenyekiti Remng’orori
Kwa upande wa Mwenyekiti wa Kijiji cha Remg’orori, Justen Mgaya Baritile alisema  mgogoro huo umedumu kwa miaka mingi.
Baritile alisema kuwa mipaka iliyokuwa ikitambulika tangu enzi hizo ni ile ya mwaka 1978 lakini umekuwa ukisusua kupata suluhisho la kudumu.

Alisema baada ya mgogoro huo kuibuka tena mwaka 1996 kulifanyika mkutano katika eneo hilo la mipaka iliyohusisha viongozi wote ngazi ya mkoa, wilaya na wananchi wa pande zote tatu hazikuafikiana.
Licha ya kutoafikiana katika mkutano huo, maafisa watendaji wa kata inadaiwa walisaini makubaliano hayo bila wananchi kuiridhia.
Baritile alisema kuwa mgogoro huo tena uliibuika mwaka 2002 ambapo  kulifanyika mkutano eneo hilo hilo na kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Serengeti Thomas Loi Sabaya (wakati huo), Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Hawa Mchopa ambaye pia alihudhuria kama Kaimu Mkuu wa mkoa wa Mara.
Alisema mkutano huo ulikaa  Februari 28 ,2002 ambapo walipendekeza kuwa mpaka wa Bunda na Serengeti utapita kuanzia mto mwikoma, Nyagubesi, Nyabetunguri, mlima bikaili hadi jiwe moja, Kewaiwai, Bonde la mtemi Makongoro hadi Mto Tirina.
Mpaka kati ya Serengeti na Musoma Vijiji walipendekeza kupita Kijiji cha Sirori Simba eneo la  Bonde la Nyagubesi, Nyabetunguri, mlima Buruta hadi palipowekwa vibao vya Tanroad barabarani kama ishara ya mwisho  wa jimbo la Musoma Vijijini.
 
Alisema kuwa licha ya kukubaliana lakini mgogoro huo uliendelea kufukuta na kulazimika tena kukaa mkutano Desemba 12, 2002 na kuhudhuria na viongozi wa ngazi kuanzia mkoa hadi kijiji ambapo waliwatumia wazee maarufu na wa kale ili kutoa historia.
Hata hivyo taarifa
Kwa Mwenyekiti (0786480194) wa Kijiji cha Sirori Simba, Alexander Makile Nyangalesi alisema kuwa maamuzi yatakayotolewa na tume yatakuwa ni sahihi.

Wassira
Kwa upande wa Mbunge wa Jimbo la Bunda (CCM), Steven Wassira alikiri kuwapo na mgogoro huo huku akienda mbali na kusema unahusisha wilaya nne yaani Serengeti, Bunda, Butiama na Msoma Vijijini.
Wassira ambaye ni Waziri wa Ofisi ya Rais, alisema migogoro yote ya wilaya hizo inahusu mipaka ambayo inapaswa kutenganisha Serengeti na Bunda, Serengeti na Musoma Vijijini na Butiama na Bunda.
Wasira alisema kuwa mipaka ya Wilaya ya Serengeti, Bunda na Butiama inahusisha vijiji vya Mikomariro, mahanga na Ikizu ambapo upande Musoma Vijijini na Serengeti unahusisha kijiji cha Sirori Simba na Remng’orori.
Pamoja na ufafanuzi wake, alisema mipaka hiyo itapata muafaka kwa kurejea historia ya tangu watawala  wa ‘machifu’ walivyokuwa wakitawala.
Wassira alipinga vikali juu ya tuhuma dhidi yake kwamba  anawatumia  matajiri  wa jimbo lake kuendeleza mapambano ya kumega ardhi ya Serengeti.
“Sina nia ya kuchukua ardhi ya Serengeti, hayo ni mawazo potofu ya wenye nia mbaya na mimi,kwanza kwenye jimbo langu sina matajiri na wananchi wangu ni wa hali ya kawaida.
“Kwanza mipaka ya wilaya hizo iliwekwa wakati mimi nikiwa Mkuu wa Wilaya, sasa kama nilikuwa na nia hiyo ningetumia mwanya huo, suala la watu kunichafua kwenye mitandao ya kijamii ni ijinga, tushirikiane kupata muafaka,”alisema.
Dk. Kebwe
Kwa upande wa Mbunge wa Serengeti, Dk. Kebwe Steven Kebwe alisema kwa ufupi kwamba ana imani na tume itamaliza mgogoro huo.
Kuhusu tuhuma za wananchi wakewakidai kushindwa kuitetea ardhi yao, alisema kuwa hatua ya tume kwenda eneo hilo ni jitihada zake na vikao vyote vya RCC kilichokaa Oktoba 17,2012 aliwatetea wananchi juu ya mipaka hiyo.

MWISHO












No comments:

Post a Comment